Erdogan aweka wazi operesheni dhidi ya IS nchini Syria.

Recep Erdogan Haki miliki ya picha Google
Image caption Rais wa Uturuki Recep Erdogan

Rais wa Uturuki Recep Erdogan ameweka wazi malengo ya operesheni ya kijeshi nchini Syria, ameeleza kuwa ngome kubwa ya kundi la wana mgambo wa IS ya Raqqa italengwa.

Uturuki hivi sasa inaunga mkono wapiganaji wa upinzani, Erdogan amesema kuwa vikosi hivyo kwanza vitakomboa mji wa Al-bab unaoshikiliwa na IS na baada ya hapo watashambulia mji wa Manbij unaoshikiliwa na wapiganaji wa Kikurd ambao wanachukuliwa kama magaidi na uturuki na watamaliza na mji wa Raqqa.

Pia rais Erdogan amesema kuwa kwa kushirikiana na Marekani, Uturuki itawaondoa wapiganaji wa dola la kiislam huko Raqqa. Lakini akasema kwamba hawahitaji msaada wowote kutoka kwa majeshi ya Kikurd.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umeonya kuwa hali itakuwa mbaya zaidi kipindi cha baridi tangu kuanza kwa vita hivyo miaka mitano iliyopita.

Afisa wa Umoja wa mataifa upande wa misaada nchini Syria Jan Egeland amesema kuwa hali itakuwa mbaya zaidi kwa waathirika wa mgogoro huo.