Jonesia Rukyaaa kuchezesha AFCON

Tanzania, CAF Haki miliki ya picha Google
Image caption Jonesia Rukyaaa Mwamuzi wa soka kutoka Tanzania

Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), limemteua Jonesia Rukyaaa - Mwamuzi wa soka kutoka Tanzania kuwa miongoni mwa waamuzi wa kati 10 watakaochezesha mechi za Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake zitakazofanyika kwa wiki mbili kuanzia Novemba 19, mwaka huu.

Kwa uteuzi huo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), amempigia simu Jonesia kumpongeza kwa hatua hiyo ambayo ni sehemu kubwa ya mafanikio ya soka la Tanzania kufanya vema katika medani za kimataifa.

Malinzi amesema kwamba Mwamuzi Jonesia ameliletea heshima taifa la Tanzania kwa kujijengea heshima ya kuaminika mbele ya Kamati ya Ufundi ya CAF - Waratibu na Waandaaji wa fainali hizo zitakazofanyika Cemaroon ambako mechi za mechi ya mwisho ya fainali itafanyika Desemba 3, mwaka huu.

"Namtakia kila la kheri, naamini kwamba Jonesia atafanya vema. Nina uhakika kwamba hii ndiyo njia yake pekee ya kufanikiwa zaidi kwani ipo siku atateuliwa kuchezesha hata fainali za Kombe la Dunia.

Jonesia anafanya idadi ya waamuzi watakaochezesha mchezo huo kutoka nchi za Afrika Mashariki kuwa watano kwa mujibu wa orodha ya CAF ni Salma Mukansanga (Rwanda), Lydia Tafesse (Ethiopia), Carolyne Wanjala (Kenya) na Suan Ratunga (Burundi).

Waamuzi wengine ni Maria Packuita wa Mauritius, Gladys Lengwe (Zambia), Akhona Zennith Makalima (Afrika Kusini), Jeanne Ekoumou (Cameroon) na Aissata Amegee (Togo). Katika orodha hiyo pia yumo Mary Njoroge wa Kenya ambaye mwamuzi wa pembeni pekee.

Katika fainali hizo, timu shiriki ni Cameroon, Afrika Kusini, Misri na Zimbabwe zipo kundi A wakati Nigeria, Ghana, Kenya na Mali zimo kundi B.