Mashirika ya UN yaitembelea Tanzania

Tanzania Haki miliki ya picha Google
Image caption Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome akitoa neno la ukaribisho kwa ujumbe kutoka nchi za Nordic ulipotembelea wizara yake jijini Dar- Es- Salaam.

Serikali ya Tanzania imeshukuru msaada mkubwa unaotolewa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kwamba taifa linakuwa na mfumo imara wa utoaji haki kwa kuzingatia demokrasia na uwajibikaji.Serikali imesema kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mifumo ya utoaji haki nchini kutokana na misaada iliyotolewa na nchi hizo kupitia Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambao unasaidia mpango huo wa UNDAP.

Hayo yameelezwa wakati ujumbe mzito wa kutoka nchi za Nordic ulipotembelea Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria. Nchi hizo za Nordic pamoja na kutoa mchango wake mkubwa katika bajeti za serikali ya Tanzania pia hutoa mchango mkubwa kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya shughuli zake nchini.

Mataifa hayo ni ya Sweden, Norway, Denmark, Finland na Iceland ambayo kwa pamoja yanaitwa mataifa ya Nordic ni wadau muhimu wa Umoja wa Mataifa na pia kwa serikali ya Tanzania.Ujumbe kutoka nchi hizo upo nchini kwa ajili ya kuimarisha mahusiano kati yao na Mashrika ya Umoja wa Mataifa yanayofanyakazi kama taasisi moja na nchi hizo (Delivering as one) kwa lengo la kuimarisha na kusukuma mbele malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Katika ziara hiyo iliyoanzia Novemba 14 wajumbe hao waliweza kuangalia utekelezaji mbalimbali wa miradi ya Umoja wa Mataifa wajumbe wa mataifa hayo wanatarajia kuzuru pia Kigoma na Dodoma .

Wakiwa Dar es Salaam, watakutana na wawakilishi wa taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali na AZAKI na pia wanatarajia kutembelea ofisi za Bunge.Taarifa iliyotolewa katika mkutano huo imesema ingawa msaada wa Umoja wa Mataifa umekuwa siku zote ukililenga eneo maalumu linaloshughulikiwa na mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa, imekuwa ni vigumu kupima athari zake katika maeneo mbalimbali yaliyokusudiwa.