Kenya yapania kuwaandikisha wapigaji kura wapya milioni 6

Tume ya uchaguzi nchini Kenya - IEBC imeanzisha leo Jumatatu shughuli ya taifa nzima ya kuwaandikisha mamilioni ya wapiga kura, kujiandaa katika uchaguzi mkuu wa Urais utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Vyama vya kisiasa nchini humo vinawarai wafuasi wao kujiandikisha kwa wakati ufao tena kwa wingi kuwa wapiga kura.

Raia nchini Kenyan watapiga kura mnamo tarehe 8 Agosti, 2017, wakati muhula wa kwanza wa Rais Uhuru Kenyatta wa miaka mitano utakapokuwa ukimalizika.

Uchaguzi huo wa mwaka huu, ni mojawepo wenye ushindani mkubwa ambapo makabila mbalimbali yanajaribu kuonyesha ubabe wao dhidi ya makabila mengine.

Tume hiyo ya Uchaguzi, The Independent Electoral and Boundaries Commission-(IEBC), inasema kuwa zoezi hilo la 'kujiandikisha kwa wingi kwa wapigaji kura' umeanza rasmi leo Januari 16 hadi Februari 14, 2017, wakati ambapo zoezi hilo litamalizika.

Tayari wakenya milioni 15.9 wamejiandikisha. Katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2013, zaidi ya watu milioni 14.4 walijiandikisha.

Maafisa wa tume hiyo ya IEBC, wanabashiri kuwa kati ya watu milioni 4 na 6 wa ziada wanalengwa katika zoezi hilo katika vituo 25,000 vya kujiandikisha kote nchini Kenya.

Mkenya yeyote wa zaidi ya umri wa miaka 18 na aliye na kitambulisho cha taifa au hati ya kusafiria, anafaa kujiandikisha baada ya kuchukuliwa alama za vidole vyake na kupigwa picha ya digirali.

Katika miezi ya hivi karibuni mkurugenzi mkuu wa IEBC Bwana Ezra Chiloba, amesema kuwa Kenya imeshuhudia "malumbano yasio na maana" na "maoni asi kuhusiana na sera ya uchaguzi mkuu" inafaa kumalizika.

"Waache wakenya wote waamue, wadau wa pande zote wanafaa kujumuika pamoja na kuhimiza raia kujiandikisha kupiga kura," Chiloba alisema.

Chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta na muungano wa upinzani NASA ambao umeundwa hivi karibuni vinawahimiza wafuasi wao kujiandikisha kwa wingi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wakenya wakisababisha ghasia mwaka 2007 wakipinga matokeo ya kura

Wiki iliyopita, vyama vitano vikuu vya upinzani nchini Kenya vilikuja pamoja na kuunda muungano wa National Super Alliance (NASA) ambao una nia ya kumuondoa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Bw William Ruto.

Muungano huo unajiandaa kumuunga mmojawao kukabiliana na chama tawala.

Uchaguzi mkuu wa mwaka 2013 ulisababisha hisia mbaya nchini Kenya, hasa baada ya kura kuwa ya ushindani mkali mno, na matokea yakiwa karibu na ukapingwa na Bwana Raila Odinga ambaye aliibuka wa pili nyuma ya Uhuru Kenyatta.

Waziri mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga amejaribu mara kadhaa kuwania kiti cha Urais bila ya mafanikio.

Mwaka 2007, Raila Odinga alishindwa na Mwai Kibaki, na kusababisha mapigano ya majuma kadhaa ya wenyewe kwa wenyewe na uhasama wa kisiasa nchini humo, ambapo karibu watu 1,500 waliuwawa, huku zaidi ya 500,000 wakiachwa bila makao.