Viti maalum kwenye ndege kuzuia unyanyasaji wa wanawake

Ndege ya abiria Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Huenda ndege nyengine pia zikatenga nafasi ya viti maalum vya wanawake.

Kampuni ya ndege ya Air India imeanza kuuza tiketi za ndege za viti vilivyotengewa wanawake pekee.

Viti sita vya mstari wa mbele katika ndege za abiria wa kipato cha wastani au 'economy' vimetengewa wanawake kufuatia ripoti za abiria wengine kuwanyanyasa baadhi ya wanawake.

Mkurugenzi mkuu kutoka kampuni hiyo ameliambia gazeti la The Hindu - kwamba wanataka kuwahakikishia abiria wanaosafiri peke yao.

Meenakshi Malik alisema: "kama kampuni kuu ya ndege nchini tunahisi ni jukumu letu kuhakikisha kuwa abiria wanawake wanasafiri kwa starehe."

Ndege hiyo pia sasa itasafiri ikiwa na maafisa wawili walinzi watakaokabiliana na abiria wasumbufu wasioweza kudhibitiwa.

Kuanzia baadaye wiki hii, iti hivyo sita vitauzwa katika ndege za Airbus A320 kwa safari za ndani nchini India.

Huenda ndege nyengine pia zikatenga nafasi ya viti maalum vya wanawake.

Lakini sio kila mtu anafurahia uamuzi huo.

Aliyekuwa afisa mtendaji wa Air India Jitendra Bhargava amesema: " Ninavyojua, hili halijashuhudiwa kokote duniani. Hakuna ukosfu wa usalama kwa wanawake katika ndege. Iwapo kuna utovu wa nidhamu, maafisa wa ndege wanaruhusiwa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria."

Sio mara ya kwanza kampuni hiyo ya ndege kukumbwa na mzozo. Mnamo mwaka 2015, wakuu wa kampuni hiyo waliwaambia baadhi ya wafanyakazi kwamba ni wanono sana kuwa wahudumu wa ndege na wanaigharimu kampuni pesa nyingi kwa kununua mafuta.