Manuel Noriega yuko katika hali mahututi

Aliyekuwa Jenerali wa Panama Manuel Noriega yuko katika hali mahututi
Image caption Aliyekuwa Jenerali wa Panama Manuel Noriega yuko katika hali mahututi

Aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa Panama, Manuel Noriega, ni mgonjwa mahututi baada ya kuvuja damu kwenye ubongo akifanyiwa upasuaji.

Bwana Noriega, mwenye umri wa miaka 83, aliachiliwa kutoka gerezani ili ajiandae kwa upasuaji huo.

Wakili wa Noriega, Ezra Angel, alisema kuwa Bwana Noriega alirudishwa katika chumba cha watu wanaougua mahututi katika juhudi za kusitisha uvujaji wa damu.

Awali madaktari walitoa uvimbe usiokuwa na saratani kutoka ubongo wake.

Alishtakiwa na kufungwa kutokana na mashtaka ya ulanguzi wa madawa ya kulevya kufuatia uvamizi wa Marekani katika Panama mwaka 1989.

Ijapokuwa hakuwa rais rasmi wa Panama, jenerali Noriega alikuwa kiungo muhimu kutoka 1983 hadi 1989 na mshirika mkuu wa Marekani katika Marekani ya kati kwa miongo minne.

Kiongozi huyo wa kijeshi wa zamani ambaye ana umri wa miaka 83 alifungwa kufuatia uvamizi wa Marekani nchini Panama 1989.

Baada ya kuhudumu kifungo cha miaka 20 nchini Marekani alisafirishwa hadi Ufaransa ambapo alifungwa miaka 7 kwa ulanguzi wa fedha.

Noriega alipatikana na hatia ya uhalifu uliofanyika wakati wa uongozi wake na kusafirishwa kutoka Ufaransa hadi Panama ili kuhudumia kifungo chake 2011.