Wakurdi 30,000 Ujerumani waandamana dhidi ya Erdogan

Haki miliki ya picha BORIS ROESSLER/DPA VIA AP
Image caption Maandamano ya Wakurdi, wakibeba bendera yenye picha ya kinara mkuu wa PKK, aliyefungwa jela Abdullah Ocalan

Zaidi ya wakurdi wa Uturuki wapatao elfu thelathini wamefanya maandamano katika mji wa Frankfurt nchini Ujerumani, dhidi ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.

Waandamanaji hao walikusanyika kutoka miji yote nchini Ujerumani, kabla ya kufanyika kwa - Nowruz, sherehe za maadhimisho ya mwaka mpya kwa Wakurdi.

Wametoa wito wa kuwepo kwa demokrasia nchini Uturuki, na wamesema HAPANA kwa shughuli za kura ya maoni ya kuongeza nguvu ya Rais, ambazo zimeandaliwa kufanyika nchini Uturuki mwezi ujao, .

Baadhi yao walipeperusha bendera huku wakibeba picha ya kiongozi wa kivita wa wakurdi aliyefungwa gerezani, Abdullah Ocalan.

Haki miliki ya picha AFP/GETTY IMAGES
Image caption Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameikashifu vikali Ujerumani

Msemaji wa Bwana Erdogan, amelaani mkutano huo na kuilaumu Ujerumani kwa upendeleo, kwa kukubalia mkutano huo kufanyika.

Baadhi ya miji kadhaa nchini Ujerumani, yalikataa kuwaruhusu mawaziri wa Uturuki kuwahutubia raia wa Uturuki walioko nchini humo.