Kutoweka kwa Roma Mkatoliki kwazua hisia Tanzania

Watu wasiojulikana wanadaiwa kuvamia studio moja ya muziki ambapo wasanii hao watatu walikuwa Jumatano jioni na kuwateka.
Image caption Watu wasiojulikana wanadaiwa kuvamia studio moja ya muziki ambapo wasanii hao watatu walikuwa Jumatano jioni na kuwateka.

Kutekwa kwa wasanii watatu akiwemo Ibrahim Musa aka Roma Mkatoliki kumezua hisia kali miongoni mwa umma.

Watu wasiojulikana wanadaiwa kuvamia studio moja ya muziki ambapo wasanii hao watatu walikuwa Jumatano jioni na kuwateka.

Zaidi ya wasanii 20 siku ya Ijumaa walikongamana katika mji wa Dar es Salaam na kufanya mkutano na vyombo vya habari huku wakishutumu kutekwa kwa wenzao huku wakitaka majibu kutoka kwa serikali.

Huwezi kusikiliza tena
Wasanii waomba usaidizi wa kumtafuta Roma Mkatoliki

Bi Nancy Mshana mkewe Roma Mkatoliki ambaye pia alikuwa katika mkutano huo aliomba usaidizi kutoka kwa vitengo vya usalama na vyombo vya habari kumtafuta mumewe.

Alilia na akalazimika kutolewa nje na mmoja wa marafikize mumewe.

''Kwa kweli nimeathirika, ni vigumu kukubali.naomba usaidizi wenu nyote ili kuhakikisha kuwa anarudi nyumbani salama'',aliomba.

Mwenyekiti wa Muungano wa wasanii nchini Tanzania Samuel Mbwana alisema kuwa hakuna habari zozote za kutia moyo zilizopatikana na polisi.

''Tunasubiri kwamba habari zaidi zitaolewa na maafisa wa polisi hivyobasi tunawaomba kuwa na subra kusubiri ripoti hiyo''.

Mmiiki wa studio ya Tongwe ambapo watatu hao walitekwa alisema kuwa watu wasiojulikana walivamia eneo hilo na kuchukua vifaa kadhaa ikiwemo kompyuta kabla ya kuondoka na Roma na wasanii wengine wawili.

''Nilipokea simu kutoka kwa shahidi mmoja mwendo wa saa moja.

Kulingana na yeye, watu waliokuwa wamevalia nguo za raia walivamia studio hiyo na kuwachukua Roma na wenzake wawili pamoja na vifaa kadhaa'', alisema.

Mashirika ya haki za kibinaadamu yalishutumu utekaji huo na kutoa changamoto kwa maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa wasanii hao wanapatikana na kwamba hakuna visa vyengine kama hivyo vitatokea.

Baadhi ya wabunge wamesema kuwa hawana raha na ukimya wa serikali.

Afisa mkuu wa Legal Human Rights Hellen KijoBisimba aliwataka maafisa wa polisi kujitokeza na kueleza, kwa sababu kuna uvumi kwamba wavamizi hao walikuwa maafisa wa usalama.