Chatu mlevi alindwa na wafungwa Australia

Chatu aliyepatikana katika mahabara

Chanzo cha picha, CORRECTIVE SERVICES NSW

Maelezo ya picha,

Chatu huyo atapata makao mapya kesi itakapokamilika

Polisi wa Australia walipovamia mahabara moja mwaka uliopita, huenda walitarajia kupata madawa ya kulevya, vifaa vya kutengeneza dawa hizo na pesa nyingi .

Lakini msako wao ulifichua kitu chengine- chatu mwenye urefu wa futi sita ambaye alionyesha dalili za kulevya. Inadaiwa mafusho ya dawa hizo na chembe chembe zake zilikuwa zimemwingia mwilini kupitia ngozi yake.

Miezi saba baadaye, nyoka huyo aliyekuwa mwenye fujo sana amerejelea hali yake ya kaawaida akiwa chini ya ulinzi wa wafungwa 14 waliochaguliwa kufanya kazi katika programu ya kuwalinda wanyama pori.

Ni mmoja kati ya wanyama 250 ambao wanalindwa katika gereza moja mjini Sydney ambalo pia lina kangaroo, wanyama tofauti na ndege wa asili.

Gereza hilo la John Morony pia linawalinda wanyama wanaotambaa mbalimbali walionaswa katika misako ya polisi.

Chanzo cha picha, CORRECTIVE SERVICES NSW

Maelezo ya picha,

Ian Mitchell, mmoja wa maafisa katika gereza wanawaoshughulikia wanyama hao

Kulingana na mmoja wa maafisa wa gereza hilo, kuna wahalifu ambao wanatumia nyoka walio na sumu kali kulinda bunduki na madawa yao ya kulevya.

Chatu huyo atapata makao mapya baada ya mahakama kukamilisha kesi dhidi ya washukiwa wa madawa ya kulevya yaliyomuathiri.

Gavana wa gereza Ivan Clader amesema programu hiyo ya kuwalinda wanyama kama hao imekuwa ikiendeshwa kwa miaka 20 sasa na imechangia pakubwa katika kubadilisha mienendo ya wafungwa.

"Tunachoona ni kuwa wanaume katika programu hii wanaopewa nafasi ya kuwalinda wanyama hawa, hubadilika na kuwa wenye utu na watulivu," alieleza BBC.

"Kuwapa wafungwa fursa hii na majukumu ya kuwalinda wanyama kunachangia pakubwa katika programu ya kuwabadilisha tabia yao."