Malala apewa tuzo ya heshima ya uraia wa Canada

Malala Yousafzai

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Malal ndiye mtu mchanga zaidi kuwahi kupokea tuzo ya heshima ya uraia wa Canada

Aliyetunukiwa tuzo ya Amani ya Nobel Malala Yousafzai anasema anashukuru kuwa mtu wa sita kupokea tuzo hiyo ya heshima ya uraia wa Canada.

Msichana huyu mwenye umri wa miaka 19 pia ndiye mtu mchanga zaidi kuwahi kupokea uraia huo.

Wakati wa sherehe rasmi huko Ottawa, Yousafzai alitoa wito kwa wanasiasa wa Canada kutumia ushawishi wao kuwasaidia wasichana duniani kote kupata elimu, ikiwa ni pamoja na wakimbizi.

Yousafzai anajulikana ulimwenguni kote kwa kupigania haki za wanawake na elimu yao.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alimsifu Yousafzai kwa utetezi wake, akisema kuwa Yousafzai ni "raia mgeni na shujaa zaidi wa Canada"

Msichana huyo wa Pakistani alitarajiwa kupata tuzo hiyo ya heshima ya uraia wa Canada mwaka wa 2014 chini ya uongozi wa aliyekuwa waziri mkuu Stephen Harper.

Hafla hiyo hata hivyo haikutendeka kufuatia kifo cha mlinzi Nathan Cirillo na ushambulizi wa bunge na Michael Zehaf-Bibeau aliyekuwa amejihami kwa bunduki.

Yousafzai aliongea kuhusu shambulizi hilo katika hotuba yake kwa wabunge wa Canada siku ya Jumatano.

"Mwanamume aliyeshambulia bunge allisema yeye ni mwislamu," alisema. "Lakini hashiriki imani yangu."

Yousafzai alisema mtu huyo alikuwa na chuki sawa na yule aliyewapiga rissasi watu sita katika msikiti mjini Quebec mwezi Januari, na yule mshambulizi ambaye aliua watu sita mjini London mwezi Machi, na wa Taliban ambao walimpiga risasi mwaka wa 2012 kwa kukaidi marufuku yao ya kuwataka wasichana kutohudhuria shule katika nchi yake ya Pakistan.

"Wanaume hawa wamejaribu kutugawanya na kuchukua demokrasia zetu, uhuru wetu wa dini, haki yetu na kwenda shule. Lakini mimi na wewe tumekataa kugawanywa, "alisema.

Vilevile aliisifu Canada kwa kuwakumbatia wakimbizi na kuendeleshaa kazi za kimataifa zilizo na maendeleo kwa wanawake na wasichana.

Watu wengine watano tu ndio wamepokea heshima ya uraia wa Canada: Nelson Mandela, Dalai Lama, kiongozi wa dini Aga Khan, mwanadiplomasia wa Uswidi Raoul Wallenberg, na kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi.

Malala aliandamana na wazazi wake Ziauddin na Toor Pekai Yousafzai.

Mapema siku hiyo ya jumatatu, Malala aliwashangaza wanafunzi wa shule ya upili ya Ottawa kwa kuwasili shuleni bila kutarajiwa na kujibu maswali yao, akiwa na mkewe waziri mkuu Sophie Gregoire-Trudeau.