Shule inayomilikiwa na wawekezaji wa Uturuki yafungwa Rwanda

jengo la shule ya sekondari ya Hope Academy
Image caption Inasemekana wamiliki wa shule ya Hope Academy ni miongoni mwa watu walio katika mtandao uliotaka kuipindua serikali ya Uturuki mwezi Julai 2016.

Serikali ya Rwanda imeamrisha kufungwa kwa shule iliyokuwa inamilikiwa na wawekezaji kutoka Uturuki. Wizara ya Elimu nchini Rwanda inasema kwamba kufungwa kwa shule hiyo ni matakwa ya serikali ya Uturuki.

Inasemekana wamiliki wa shule hiyo ni miongoni mwa watu walio katika mtandao uliotaka kuipindua serikali ya Uturuki mwezi Julai 2016.

Kulingana na wizara ya elimu ya Rwanda, shule ya sekondari ya Hope Academy Rwanda mepewa hadi ifikapo Ijumaa wiki hii kuwa imefunga milango.

Waziri wa elimu Papias Musafiri Malimba amesema kwamba uamuzi huo ni matakwa ya serikali ya Uturuki: "Serikali ya Uturuki ilituomba shule hii iwe chini ya mamlaka yake badala ya kuwa shule ya kibinafsi. Sisi tuliona kwamba hilo haliwezikani kutokana na mkataba tuliokuwa nao. Sisi tuliamua kuifunga ili kutekeleza matakwa ya serikali ya Uturuki. Kinachobaki labda ni wao wenyewe kuelewana." Alisema Waziri Musafiri Waziri Musafiri aliongeza kuwa, hatma ya wanafunzi itakuwa kwamba watatafutiwa shule nyingine zenye hadhi ya shule hiyo.

Mwandishi wa BBC nchini Rwanda Yves Bucyana aliyeitembelea shule hiyo anasema, shule hiyo ya kifahari imejengwa pembezoni mwa jiji la Kigali.

Image caption Wazazi wengi walionekana ndani ya vioo vyeusi vya magari yao wakiwa na nyuso za kukata tamaa wallipoingia kuchukua alama za watoto wao

Licha ya kunyimwa kibali cha kuingia ili kujua hali halisi ya uamuzi huu aliweza kutambua kuwa wazazi waliwakuwa wakiingia shuleni hapo kuchukua alama za watoto wao ambao tayari wameanza likizo.

Wazazi wengi walionekana ndani ya vioo vyeusi vya magari yao wakiwa na nyuso za kukata tamaa.

Mmoja wao ambaye alikubali kuzungumza na BBC alisema:" Mtoto wangu anasoma mwaka wa pili wa shule za chekechea, binafsi nimepigwa na bumbuwazi kutokana na uamuzi huu. Ni jambo la kusikitisha hasa kutokana na kwamba wengi wetu walikuwa wamekwishalipa ada ya masomo ya mwaka mzima. Mimi nililipa franga zaidi ya milioni mbili unusu za Rwanda ni kama dolla elfu mbili na mia tano(2.500) za Marekani. Nasikia kichwa kimevurugika bado hatujajua la kufanya"

Shule ya sekondari ya Hope Academy inafwata mitaala ya masomo ya Cambridge.

Nchi ya Uturuki ina uhusiano wa kideplomasia na kibiashara na Rwanda ambapo wafanyabiashara wengi kutoka Uturuki wamewekeza sana nchini Rwanda hususan katika sekta ya elimu.