Watu kadhaa wameuwawa Orlando, Marekani

Eneo la tukio limezingirwa na maafisa wa polisi huko Orlando

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Eneo la tukio limezingirwa na maafisa wa polisi huko Orlando

Idara ya Polisi huko Florida inasema kuwa watu kadhaa wameuwawa katika kisa cha ufyatuliaji risasi katika eneo la viwandani huko Orlando, Marekani.

Kisa hicho kilifanyika mapema Jumatatu asubuhi, mashariki mwa mji huo, gazeti la Orlando Sentinel, limeripoti.

Kinatukia wiki moja kabla ya maadhimisho ya mwaka wa kwanza ya shambulio katika klabu moja ya usiku ya Pulse mjini humo, ambapo watu 49 waliuwawa.

Polisi wanasema kwamba eneo la tukio hilo ''limezingirwa'', ikiwa na maana kuwa hakuna makabiliano yanayoendelea kwa sasa.

Afisa mkuu wa polisi katika kaunti ya Orange, anatarajiwa kutoa taarifa kwa waandishi habari muda mchache ujao.

Maelezo ya picha,

Ramani ya Marekani

Duru kutoka Florida, zinasema kuwa mauwaji hayo yametokea katika eneo moja la biashara ya kuunda hema na vifaa vya kupiga kambi, huku ikisemekana kuwa maafisa wa shirika la upelelezi- FBI wamefika eneo la tukio.

Katika shambulio la Juni mwaka jana, mauwaji mabaya zaidi ya ushambuliaji wa risasi katika historia ya miaka ya hivi karibuni, muuwaji kwa jina Omar Mateen, aliwamiminia risasi na kuwauwa watu 49 huku akiwajeruhi wengine kadhaa, katika klabu moja ya usiku ya wapenzi wa jinsia moja, kabla ya kuuliwa na polisi baadaye.