Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari anaendelea 'kupata nafuu'

Rais Buhari alidokeza kuwa aliongezewa damu Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Buhari alidokeza kuwa aliongezewa damu

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari "anaendelea kupata nafuu haraka" kutokana na ugonjwa alio nao, mkewe Aisha Buhari amesema.

Mke huyo wa Rais amaesema hayo, baada ya kuzuru London, mahali ambapo mumewe anaendelea na matibabu kutokana na ugonjwa ambao bado haujatajwa.

Bw. Buhari, 74, alipelekwa hospitalini jijini London mwezi mmoja uliopita, kwa ziara yake ya pili ya matibabu nchini Uingereza mwaka huu.

Kukosekana kwake uongozini kumesababisha mihemko nchini Nigeria, taifa lenye uchumi mkubwa na idadi kubwa ya watu barani Afrika, huku baadhi ya watu wakiteta kuhusiana na iwapo ataweza kurejelea kazi yake tena.

Naibu wa Rais Yemi Osinbajo anatumika kama kaimu, na amesifiwa pakubwa kwa namna anavyoshughulikia mzozo wa kiuchumi, hasa baada ya kushuka kwa bei ya mafuta, bidhaa muhimu inayouzwa kwa wingi nje ya nchi.

Image caption Bi Aisha Buhari, Mkewe Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari

Mwezi Januari mwaka huu, Bwana Buhari alichukua wiki saba ya likizo ya matibabu kwenda Uingereza.

Aliporejea nyumbani mwezi Machi, alisema kuwa ameongezewa damu, lakini hakufichua ni ugonjwa gani anaougua.

Alirejea tena Uingereza mnamo Mei 7, kwa matibabu zaidi.

Mkewe sasa amesema kuwa mumewe "anahitaji maombi ya kila mara na hivi karibu ataweza kujiunga na raia wake tena, kwani anaendelea kupona haraka.".

Amerejea nchini Nigeria baada ya kuwa na mumewe huko London hospitalini kwa muda wa wiki nzima.

Buhari alianza kuugua 2017

Januari 19: aliondoka Nigeria kwenda Uingereza "kwa likizo ya kimatibabu"

Februari 5: akaliomba Bunge kumuongezea likizo ya kimatibabu

Machi 10: Alirejea nyumbani lakini hakuingia kazini

Aprili 26: Akakosa kuhudhuria mkutano wa baraza la mawaziri na akasema "nafanyia kazi nyumbani"

Aprili 28l: akakosa maombi ya Ijumaa

Mei 3: Akakosa mkutano wa tatu mtawalio wa baraza la mawaziri

Mei 5: Akaonekana katika swalah ya Ijumaa mjini Abuja

Mei 7: Akasafiri hadi Uingereza kwa matibabu zaidi

Juni 6: Aisha Buhari akasema 'anapona haraka'