Watoto 2 wapatikana wakiwa hai katika shambulio la al Shabaab Kenya

Image caption Wanamgambo wa Al Shabaab wametekeleza mashambulio kadhaa ya ugaidi nchini Kenya

Wanafunzi 2 kati ya 4 walioripotiwa kutoweka mapema wiki hii, baada ya gari la polisi kulipuliwa na bomu lililotegwa barabani katika msitu wa Boni pwani ya Kenya, wamepatikana.

Lori la polisi wakulinda amani mpakani RBPU iliyokuwa imewabeba maafisa wa polisi 20 na wanafunzi wa shule 14 lililokuwa njiani kwenda maeneo ya Kiunga Wilayani Lamu, lilikanyaga kilipuzi na kulipuka na kusababisha vifo vya maafisa 4 wa polisi na wanafunzi 4, ilihali wanafunzi 5 hawakujilikana waliko.

Kwa mjibu wa vyombo vya habari nchini Kenya, na kiongozi wa kaunti ndogo ya Lamu Mashariki Shee Kupi, mtoto mmoja alipatikana msituni Jumanne usiku ilihali mwanafunzi wa pili akapatikana jana Jumatano.

Wote wawili wanasemekana wana majeraha mabaya na wako katika hali mahututi.

Wapiganaji wa Al Shabaab, wamekiri kutekeleza shambulio hilo.