Viongozi wa Afrika wakemewa na kuitwa 'Watalii wa kiafya'

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari akishuka ndege baada ya kurejea nchini mwake mwezi huu wa Agosti baada ya kuwa London, Uingereza kwa likizo ya siku 100 ya matibabu Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari akishuka ndege baada ya kurejea nchini mwake mwezi huu wa Agosti baada ya kuwa London, Uingereza kwa likizo ya siku 100 ya matibabu

Waziri mmoja nchini Afrika Kusini, amewakosoa vikali viongozi wa Bara Afrika ambao wanakwenda ng`ambo kutafuta matibabu.

Aaron Motsoaledi amewalaani viongozi hao na kuwaita "Watalii wa kiafya". Amesema hayo akiwa Zimbabwe.

Rais Robert Mugabe, ambaye mara kwa mara anapokea matibabu nchini Singapore, alikuwa ameondoka kutoka katika, mkutano huo unaohudhuriwa na mawaziri wa afya, ndipo Dkt Motsoaledi, alipotoa matamshi hayo.

Msemaji wa Bwana Mugabe, alikuwa amesema kuwa Daktari wa kibinafsi wa Rais Mugabe ''sio tu raia wa Zimbabwe," ni mtu mweusi.....Na ni mweusi, mweusi mweusi sana".

George Charamba, alsema hayo alipokuwa akihojiwa na gazeti la serikali ya Zimbabwe - The Herald, mwezi Mei mwaka huu, akisisitiza kuwa Rais Mugabe kamwe haipi kisogo sekta ya matibabu ya nchini hiyo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa Angola José Eduardo dos Santos

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na mwenzake wa Angola José Eduardo dos Santos pia wamekosolewa vikali kwa kutafuta matibabu nje ya nchi mwaka huu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais aliyetawala Zimbabwe kwa muda mrefu zaidi Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka 93

Katika kongamano hilo wiki hii Dr Motsoaledi alisema:

"Sisi ndilo bara pekee duniani, ambalo viongozi wake wanatafuta matibabu matibabu katika mataifa ya kigeni yaliyoko nje ya bara hili, nje ya eneo letu. Inafaa tuaibikia hilo."

"Hii inaitwa utalii wa kiafya. Tunafaa kuboresha na kupigia debe kilicho chetu," aliongeza.

Dkt Motsoaledi pia ameiomba mataifa ya Afrika kuongeza ufadhili wa kifedha kwa sekta ya matibabu.

Amepongezwa mno na raia nchini Afrika Kusini kwa kutumia hospitali za umma badala ya hospitali za kibinafsi.

Uchambuzi: Shingai Nyoka, BBC Victoria Falls, Zimbabwe

Orodha ya majina ya Marais wa Afrika waliokwenga ngambo kwa matibabu ni:

  • Robert Mugabe, Zimbabwe
  • Muhammadu Buhari, Nigeria
  • José Eduardo dos Santos, Angola
  • Patrice Talon, Benin
  • Abdelaziz Bouteflika, Algeria

Wakati Dkt Motsoale, alipotoa matamshi hayo wakati wa vikao vya kongamano hilo, kulikuwa na ukimya kutoka kwa wanachama wa mataifa yaliyowakilishwa.

Dkt Motsoaledi alikiri kuwa msimamo wake una utata, lakini aliamua kusema kindakindaki.