Polisi Tanzania wawashikilia watu 12 kwa tuhuma za mapenzi ya jinsia moja

Mapenzi ya jinsia moja ni makosa ya jinai katika nchi nyingi barani Afrika
Image caption Mapenzi ya jinsia moja ni makosa ya jinai katika nchi nyingi barani Afrika

Polisi nchini Tanzania wanaendelea kuwashikilia watu 12 wanaodaiwa kusambaza itikadi za mapenzi ya jinsia moja.

Awali kundi hilo lilikamatwa wiki iliopita na baadaye kuachiwa kwa dhamana.

Lakini siku ya Jumamosi watu hao walikamatwa tena.

Miongoni mwa waliokamatwa ni raia wa Afrika Kusini wawili na Mganda mmoja ambao wanashikiliwa katika kituo kikuu cha polisi jijini Dar es salaam wakisubiri kushtakiwa.

Wakili wao, Jebra Komble ameiambia BBC kuwa kundi hilo lilikamatwa likifanya mkutano kuhusu namna ya kuishtaki serikali kwa kuvifungia vituo kadhaa vya afya vilivyokuwa vikitoa huduma za afya kwa wapenzi wa jinsia moja.

Kukamatwa kwa kundi hili ni muendelezo wa kampeni ya serikali katika kudhibiti shughuli zinazohusisha mapenzi ya jinsia moja nchini Tanzania.

Siku za hivi karibuni, serikali ya Tanzania ilifanya msako dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, ambapo mnamo mwezi Septemba 2016, serikali ilisitisha kwa muda miradi ya Ukimwi inayolenga watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Mnamo mwezi Februari, serikali ilisitisha huduma za vituo 40 vya afya vya kibinafsi kwa madai kwamba vilikuwa vikitoa huduma kwa wapenzi wa jinsia moja.

Mapenzi ya jinsia moja miongoni mwa wanaume ni kosa la jinai nchini Tanzania na hatia yake inaadhibiwa kwa kifungo cha kati ya miaka 30 au maisha jela.

Mada zinazohusiana