Rais wa Cameroon aadhimisha miaka 35 uongozini

Paul Biya alisomea sheria katika Chuo cha Sorbonne Mjini Paris, Ufaransa

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Paul Biya alisomea sheria katika Chuo cha Sorbonne Mjini Paris, Ufaransa

Leo Jumatatu Rais wa Cameroon Paul Biya, anaadhimisha miaka 35 uongozini na kumfanya kuwa Rais aliyehudumu kwa miaka mingi zaidi barani Afrika.

Bwana Biya aliingia kwa mara ya kwanza uongozini mwaka 1982, wakati taifa hilo lililikuwa chini ya mfumo wa utawala wa chama kimoja.

Hata hivyo, licha ya taifa hilo kwa sasa liko katika mfumo wa uongozi wavyama vingi vya kisiasa, amefaulu kusalia mamlakani kwa miaka hii yote.

Mnamo mwaka 2011, baada ya katiba ya taifa hilo kunayiwa mabadiliko yenye utata ya kumruhusu kuwania kiti cha Urais tena, alifaulu kushinda tena uchaguzi mkuu kwa asilimia 78 ya kura zote zilizopigwa na kusalia mamlakani kwa miaka mingine saba.

Ushindi huo mkubwa, uliwafanya wakosoaji wake wengi kuhoji na kushuku uhalali wa uchaguzi huo.

Bwana Biya ni sehemu ya kundi la viongozi kadhaa Afrika, ambao wametawala mataifa yao kwa zaidi ya miaka 30: Wao ni pamoja na Robert Mugabe wa Zimbabwe na Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa taifa dogo la Equatorial Guinea, ambao wangali wakishikilia mamlaka.

Bwana Biya mwenye umri wa miaka 84, na ambaye wakosoaji wake wanamtuhumu kwa kuongoza taifa kiimla, anatarajiwa kuwania tena kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu mwaka ujao wa 2018.

Unaweza kupata mengi kumhusu Bw. Biya hapa.