Wengi wamefariki baada ya makabiliano ya risasi, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria

Wanamgambo wa Boko Haram nchini Nigeria
Maelezo ya picha,

Wanamgambo wa Boko Haram nchini Nigeria

Maafa na majeruhi mengi yametangazwa kufuatia makabiliano makali ya risasi kati ya jeshi la Nigeria na washukiwa wa kundi la wapiganaji wa kiislamu wa Boko Haram, katika mji wa Gulak ulioko kwenye jimbo la Adamawa, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Wanamgambo hao walitekeleza shambulio usiku wa kuamkia Jumanne na kuwalazimisha mamia ya raia kukimbilia maeneo ya milimani.

Idadi ya waliouwawa hadi kufikia sasa bado haijajulikana, na idadi hiyo inajumuisha walinda usalama, raia na wapiganaji hao wa Boko Haram.

Wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa Boko Haram ndio waliokuwa wa kwanza kushambulio kijiji kimoja kilichoko karibu, kabla ya kusonga mbele na kuufikia mji wa Gulak.

Walikabiliwa vikali na wanajeshi wa taifa la Nigeria pamoja na makundi ya wapiganaji wa kiraia, ambapo makabiliano yalidumu saa kadhaa.

Shambulio hilo linatukia saa 24 tu, baada ya wahanga wawili wa Boko Harama kujilipua, na kuwauwa watu wawili katika eneo moja lililoko mpakani na Cameroon.

Mashambulio hayo yanaonesha kuwa wanamgambo wa Boko Haram bado ni tishio kwa usalama katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, licha ya jutihada kubwa zinazofanywa na jeshi la utawala wa Nigeria katika makabiliano dhidi ya wauwaji hao.