Grace Mugabe anaweza kuwa ametorokea Namibia?

Grace Mugabe Haki miliki ya picha AFP

Mbunge wa upinzani nchini Zimbabwe Eddie Cross ameambia BBC kwamba anaamini mke wa Rais Mugabe, Grace, ametorokea Namibia.

Mwanasiasa huyo wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) amesema anafahamu kwamba Grace aliruhusiwa kuondoka nchini humo usiku wa kuamkia leo na jeshi.

Ameongeza kwamba alikuwa hana kwingi kwa kwenda kutafuta hifadhi baada yake kudaiwa kumdhalilisha mwanamitindo Afrika Kusini jambo lililomaanisha kwamba hawezi kuwa salama huko.

Hata hivyo, taarifa hizi hazijathibitishwa na jeshi.

Kwenye taarifa rasmi kwenye runinga ya taifa awali, Meja Jenerali Sibusiso Moyo alihakikishia taifa hilo kwamba rais na familia yake walikuwa salama na usalama wao ulikuwa umehakikishwa.

Taarifa hiyo ilionekana kuashiria kwamba huenda familia ya rais ilikuwa inazuiliwa kwa pamoja nyumbani kwao Harare.

Nick Mangwana, mwakilishi wa chama tawala cha Zanu-PF nchini Uingereza ameambia BBC kwamba mwenyewe pia amepokea taarifa kwamba Grace hayupo tena nchini Zimbabwe.

Lakini Bw Mangwana amesema katika siasa za Zanu-PF, Bi Mugabe ni mtu wa chini sana na hana usemi wowote.

Amesema ana mamlaka tu kwa sababu ya kuwa ni mke wa Rais Mugabe.

"Alichukua wadhifa wa juu kuliko ule anaostahiki kuwa nao," amesema.

Bi Mugabe amekuwa akitaka kuwa makamu wa rais, na sasa kwa sababu ameongoka, chama hicho kinaweza kufanya mkutano wake mkuu bila kuingiliwa.

Amekiri kwamba si kawaida kwa jeshi kuchukua mamlaka katika nchi inayoongozwa kidemokrasia lakini kwamba hali haijakuwa ya kawaida Zimbabwe.

"Tuna rais wa miaka 93, na hilo si jambo la kawaida, na hatuna sarafu yetu pia," amesema.

Lakini amesema kirasmi Rais Mugabe bado yumo kwenye usukani kwani jeshi halijasitisha utekelezwaji wa katiba na kwamba taifa hilo bado lina serikali ya kiraia.

Amesema rais Mugabe aliongoza mkutano wa baraza la mawaziri jana jioni kama kawaida.

Haki miliki ya picha AFP

Grace Mugabe ni nani na mbona kuinuka kwake kunakumbwa na utata?

  • Alianza uhusiano na Robert Mugabe, ambaye ni mkubwa kwake kwa miaka 41,akifanya kazi kama mpiga chapa katika ikulu.
  • Bw Mugabe baadaye akasema kuwa mke wake wa kwanza Sally, ambaye alikuwa mgonjwa wakati huo alifahamu na kuidhinisha uhusiano huo.
  • Aliolewa na Mugabe, mume wake wa pili mwaka 1996 kwenye sherehe kubwa. Wana watoto watatu.
  • Alipewa jina (Gucci Grace) na wakosoaji wake kwa matumizi yake ya pesa nyingi kwa anasa.
  • Yeye na mume wake wakewekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya na Marekani vikwemo vya usafiri.
  • Kwa njia ya utata alipata shahada ya PhD mwezi Sepetemba mwaka 2014 baada ya miezi miwili tu.
  • Aliteuliwa mkuu wa kitengo cha wanawake cha Zanu-PF mwaka 2014. Aliliumiwa na mwanamitindo wa Afrika Kusini kwa kumpiga Agosti mwaka 2017.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii