Klopp 'akasirikia' mpangilio wa kikosi chake kabla ya mkwaju wa Willian

Willian sasa amefunga mabao matau katika mechi nne alizocheza Haki miliki ya picha PA
Image caption Willian sasa amefunga mabao matau katika mechi nne alizocheza

Meneja wa Klabu ya Liverpool Jurgen Klopp amesema amekasirishwa na kikosi chake kushindwa kufanya mabadiliko kabla yamchezaji Willian kusawazishia Chelsea katika mechi waliyotoka sare ugani Anfield.

Klopp alikuwa akijaribu kumuingiza Adam Lallana wakati Willian, ambaye alifunga mara mbili dhidi ya Qarabang kwenye mechi ya klabu bingwa barani Uropa siku ya Jumatano, alipofunga bao katika dakika ya 85 na mkwaju uliopita juu ya mlinda lango Simon Mignolet.

''Nilikasiriswa kwa kuwa tulitaka kubadili mfumo wetu ila mwamuzi hakutupa nafasi hiyo,''Mjerumani huyo alieelezea runinga ya BT Sport.

'' Sijui alichokuwa akifikiria wakati huo,alinieleza kuhusu sisi kuchukua muda sana na hilo sielewi.

''Tunawezaje kuchukua muda mrefu?Hatukutaka kuharibu wakati,tulitaka kubadili mfumo na hiyo ndo sababu iliyonikasirisha.''

Bao la Willian lilimnyima Mohamed Salah matokeo ya aliyokuwa akiotea dhidi ya klabu yake ya jadi baada yake kutia kimyani bao la kwanza kwenye mechi hiyo.

Salah sasa amefunga mabao kumi katika mechi 13 kwenye ligi ya Premier ya Uingereza msimu huu na Mmisri huyo amekuwa moto wa kuotea mbali tangu kujiunga na Liverpool.

Salah alikuwa na nafasi ya kuishindia Liverpool mechi hiyo katika dakika ya mwisho ya mchezo ila mkwaju wake ulizuiliwa na Thibaut Courtois.

Chelsea hawajapoteza hata mechi moja katika mechi saba ugani Anfield tangu mwaka 2013.

Mada zinazohusiana