Wakimbizi Warundi kupata Vitambulisho vya kisasa Rwanda

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi imefadhili zoezi hilo
Image caption Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi imefadhili zoezi hilo

Serikali ya Rwanda imeanza zoezi la kusajili upya wakimbizi kutoka Burundi miaka tatu tangu wakimbilie nchi humo.

Usajili huo unafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa, vifaa maalum vikinasa alama za macho na vidole.mwishowe kila mmoja atapatiwa kitambulisho cha kielectroniki chenye data zinazomhusu yeye na watu wa familia yake.

Zoezi limeanzia mjini Kigali ambako kuna wakimbizi wanaokadiriwa kuwa elfu 30.

Zoezi hilo linalodhaminiwa na shirika la umoja wa mataifa la wakimbizi linalenga kuwapa vitambulisho vya kielectroniki ili kuwa rahisishia kuishi maisha ya kawaida nchini Rwanda pamoja na kufanya kazi ama kuwa huru kutembea katika mataifa ya kigeni.

Image caption Nukuu ya mmoja wa wakimbizi aliyekuwa akisubiri kupata kitambulisho

Serikali pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wanasema usajili huu wa wakimbizi kutoka Burundi utasaidia kujua idadi kamili ya wakimbizi hao waliotoroka nchini humo miaka 3 iliyopita.

Awali walikadirika kuwa elfu 84,idadi ambayo pande mbili zinasema imebadilika kwa sasa.

Image caption Kuna zaidi ya wakimbizi 150,000 wa kutoka Burundi na DRC nchini Rwanda

Kwa mujibu wa Waziri wa Rwanda anayehusika na maswala ya wakimbizi, Bi Jeanne d'Arc de Bonherur, utaratibu huu unakuja kutatua tatizo la wahamiaji haramu wanaojisajili kama wakimbizi katika nchi nyingi.

"Tutaweza kupata idadi rasmi ya wakimbizi baada ya baadhi kuzaliwa,wengine kuhamia katika mataifa mengine na wengine kufariki.hii itatusaidia kuratibu mipango ya kuwasaidia." alisema Bonherur

Akizungumza na mwandishi wa BBC Yves Bucyana, Waziri alielezea "Kadi hii itawasaidia kujisikia huru nchini,kuhudumiwa kama wananchi,haki ya kupata kazi na mikopo ya benki na kubwa zaidi itasaidia kuondoa tabia mbaya ya baadhi ya wakimbizi kujisajili katika nchi nyingi."

Rwanda na Shirika la wakimbizi duniani wanasema kwamba zoezi hili litakuwa limeshakamilika mnamo miezi 7 kwanzia sasa.

Rwanda inahesabu wakimbizi wapatao laki moja unusu kutoka nchi za Burundi na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wakimbizi kutoka DRC tayari wameshasajiliwa na kupewa vitambulisho vya kielektroniki.

Mada zinazohusiana