Lupita: sikuwahi kusikia hata filamu moja ya ushujaa yenye watu weusi

Nyota wa filamu Black Panther, Lupita Nyong'o katika uzinduzi wa filamu hio Ulaya

Chanzo cha picha, Tim P. Whitby/Getty Images

Maelezo ya picha,

Nyota wa filamu Black Panther, Lupita Nyong'o katika uzinduzi wa filamu hio Ulaya

Filamu ya Black Panther bado inaendelea kuwa gumzo. Leo hii imezinduliwa jijini Johannesburg Afrika Kusini na sehemu menignio barani Afrika .

Filamu hii inahusu mji wa kufikirika wa Kiafrika na imesheheni waigizaji wenye asili ya Afrika.

Mwandishi wa BBC Kim Chakanetsa amezungumza na mmoja wa nyota wa filamu hiyo Lupita Nyong'o. Alianza kwa kumuuliza kwanini ni muhimu kwake kushiriki katika filamu hii?

Lupita: Tangu mwanzo kabisa wakati Ryan aliponiambia juu ya maudhui ya filamu hii, sikuamini - sikuwahi kuskia hata filamu moja ya ushujaa ya namna hii. Nikamuuliza "Una uhakika Marvel wamekubaliana na simulizi hii? Akasema ndio ndio, wamekubali. Kikubwa katika filamu hii ni kwamba haijaogopa kugusia masuala ya msingi na ya kina ya kijamii na kisiasa na kwa kweli inaendana kabisa na ulimwengu wetu huu wa leo

Kim: Huko nyuma palikuwa na malalamiko jinsi gani ambavyo Afrika inaonyeshwa kwenye filamu. Unadhani kwa filamu hii ya Black Panther ni ishara kwamba mambo yanabadilika na mtazamo juu ya Afrika unabadilika?

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wacheza sarakasi wakisimama karibu na picha ya Lupita Nyong'o katika uzinduzi wa Black Panther Kisumu, Kenya

Lupita: Kile ambacho Black Panther inaonesha ni namna gani kuna watu wengi ambao wanaelewa upotoshwaji ambao Afrika imekuwa ikifanyiwa. Unajua mara nyingi bara la Afrika linapoonyeshwa kwenye sinema, inakuwa ni kwa ujumla sana na sote tunalazimishwa kuendana na ujumla huo. Kwahivyo kwasababu nchi yetu ya kufikirika ya Kiafrika inazungumza lugha ya IsiXhosa, tulihitaji kujifunza hiyo lugha, tulihitaji hata kutumia rafudhi yake katika Kiingereza. Tulitia nguvu sana kwenye vitu kama hivyo. Hata kule kuwakilisha tu mila fulani. Kila kitu, hata kama ni juu ya nchi ya kufikirika ya Kiafrika, inahuishwa na kuwa ya kweli kutoka mila za kweli au halisi za Kiafrika.

Chanzo cha picha, TONY KARUMBA/Getty Images

Maelezo ya picha,

Baba yake Lupita Nyong'o, Dr. Anyang Nyong'o akipiga pose karibu na shabiki aliyevaa kama muhisika kuu wa filamu ya Black Panther

Kim: Na labda wakati unakua, ulikuwa ni mpenzi wa vitabu vya katuni?

Lupita: Siwezi kusema kwamba nilikuwa ni mpenzi kiviiilee, ndio nilisoma vitabu kama Archie, Asterix [Kim: haha] Na vingine kama hivyo yaani. Nilikuwa naangalia pia sinema za mashujaa na vitu kama hivyo. Lakini sio kwamba nilikuwa ni mpenzi saana wa vitabu vya katuni

Kim: Kweli? Kuna kitabu unachokipenda cha katuni?

Lupita: Napenda kitabu cha Brian K. Vaughan's kina kichwa cha habari 'Why The Last Man', ambacho ndio nimekimaliza muda si mrefu