Vikosi vya Nigeria vyashindwa kumkamata Shekau

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau
Maelezo ya picha,

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau

BBC imebaini kuwa hivi karibuni vikosi vya jeshi la Nigeria vilishindwa kumkamata kiongozi wa kundi la wapiganaji wa Boko Haram Abubakar Shekau katika operesheni maalum iliyofanyika

Video ambayo BBC imepewa inawaonyesha wanajeshi wa Nigeria wakiielekea kambi ya Shekau katika misitu ya Sambisa Kakskazini mashariki mwa Nigeria.

Hata hivyo baada ya siku nne kuielekea ngome ya Shekau kaskazini mashariki mwa Nigeria,wanajeshi hao waliamriwa kusitisha safari yao ya kusonga mbele.

Hata hivyo muda mfupi baadaye askari hao wa vikosi vya serikali ya Nigeria ghafla walishambuliwa na wapiganaji ambao walitumia gari lililokuwa limejaa vilipulizi.

Katika shambulio hilo la kujihami kutoka kwa kundi hilo la Boko Haram dhidi ya vikosi vya serikali lilisababisha vifo kwa wanajeshi saba miongoni mwao wakiwa ni kutoka Nigeria na Cameroon

Hadi vikosi vya Nigeria vinajipanga upya tayari inadaiwa kuwa Shekau,alitumia mwanya huo kutoroka.

Serikali ya Nigeria wiki iliyopita imetangaza zawadi ya dola elf nane kwa mtu atakatoa taarifa za kuwezesha kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kundi la Boko Haram Abukbakar Shekau

Kundi hili la wapiganaji lililowahi wateka wanafunzi wasichana zaidi ya 200 wa Chibok limefanya tena jaribio la kutaka kuwateka wanafunzi na walimu Kaskazini mwa Nigeria.