Kina baba watano wazungumzia sifa bora za baba Tanzania

Miongoni mwa picha za baba bora katika onesho
Image caption Miongoni mwa picha za baba bora katika onesho

Mifumo mingi ya maisha katika jamii za kiafrika, kwa mujibu wa mila na desturi majukumu ya malezi ya watoto yanaachwa kwa mwanamke huku wanaume wakiona kana kwamba si jukumu lao.

Hivyo kutokana na mitazamo hiyo, ubalozi wa Sweden nchini Tanzania umeandaa mpango maalumu unaotumia picha ili kuwahamasisha wanaume kuachana na dhana hiyo ya kutokuwa na usawa katika malezi ya watoto katika familia.

Baba wa aina fulani huwa anategemea na tamaduni na jamii husika na uamuzi wa maisha ya baba huyo.Na inawezekana kuwa hakuna usawa katika kuwalea watoto nyumbani kutokana na tamaduni.

Nchini Tanzania kwa mwanaume kukutwa akimbadilisha nguo mtoto,ni jambo linaloweza kuzusha mjadala,ambapo katika jamii nyingine mwanaume huyo hutuhumiwa kama kapewa dawa za kupumbazwa akili maarufu kama Limbwata.

Pamoja na kwamba baadhi ya wasanii wa maigizo wamekuwa wakilionyesha uzito wa jambo hili kupitia tungo zao,lakini bado wapo ambao wanaamini kuwa hakuna mpaka kati ya kazi za baba na mama katika suala la malezi ya watoto.

Single Mtambalike maarufu kama Richie Richie ni muigizaji wa filamu nchini Tanzania na katika onyesho hilo ametambuliwa kuwa ni miongoni mwa baba bora nchini humo.

Haki miliki ya picha Ubalozi wa Sweden
Image caption Ametunukiwa tuzo ya Baba bora nchini Tanzania

Richie anasema ukiachia nafasi yake ya kuigiza ambayo inamtaka kuigiza kulingana na kile ambacho kipo kwenye hadithi ili filamu ifanye vizuri katika soko lakini ukija kwenye maisha ya uhalisia yeye ni baba .

Anatamani kuwepo na tungo ambazo zinatoa elimu sio tu biashara.

Licha ya umaarufu alionao nchini kwake,anasema umaarufu wa kucheza filamu ni kazi kama kazi nyingine,''haunizuii mimi kupanga mastari ninapokuwa na watoto wangu hospitalini''.

Kutokana na kukua kwa teknolojia Richie anasema kuna umuhimu kujua kama mtoto wako anafuatilia mtu fulani au vitu fulani ili mwisho wa siku ujue anataka kuwa nani na sio kupoteza muda,

mwanangu atamfuatilia Ronaldo labda kama anataka kuwa mcheza mpira au kufuatilia mwanamuziki kama anatamani kazi hiyo lakini kama hiyo sio ndoto yake hakuna umuhimu wa kutumia nguvu nyingi huko.

Image caption Baba wa watoto watano,Mcheza soka wa zamani,Omary Gumbo

Omary Shabani Gumbo mwenye umri wa miaka 71, alikuwa mwanasoka wa zamani nchini Tanznia aliyekuwa anachezea timu ya simba.

Yeye ni baba wa watoto watano na anasema ameshiriki katika kuleta furaha katika familia kwa kuchukua jukumu la kuwalea wanawe wote mara tu wanapozaliwa.

"Siku zote arobaini za mwanzo, jukumu la malezi ni mimi , kuanzia kuvalisha nepi,kuogesha na kubembeleza,mama kazi yake ni kula na kunyonyesha tu. ''

''Usiku wote ninakesha na mwanangu na asubuhi naamka nikwenda mazoezini na kazini pia naenda licha ya kuwa sikuwa na mapumziko lakini niliweza na utashi huo unanifanya nijione kuwa ni baba

niliyefanya majukumu yangu na heshima katika familia inakuwepo.

Image caption Onyesho la picha la baba bora wa kiswidi na kitanzania

Erick Luyange ana watoto wawili,yeye alivutiwa kufika katika onesho hilo,anasema anavutiwa kuona utamaduni wa kulea mtoto na zinaonyesha kuwa baba ni sehemu ya malezi ya mtoto nyumbani katika kumlisha,kumuogesha na mengine mengi.

Tofauti na mila zetu za kiafrika ambapo mtoto akizaliwa ni jukumu la mama wakati wenzetu baba anahusika zaidi na makuzi ya mtoto,kujenga hisia kwa mtoto ni muhimu sana.

Hii imenionyesha kuwa hata kile ambacho mimi na mke wangu tunaifanya na hata watu wanatushangaa kuwa ni sawa,Mimi na mke wangu tumewekeana ratiba na mimi ratiba yangu ya ulezi ni jumanne,alhamisi,na jumapili siku nzima.

Majukumu yangu ni kuanzia kuwaogesha,kuwalisha ,kuwapeleka sinema na kuogelea na mara nyingi huwa naenda nao hata kwenye vikao vyangu vya kibiashara.

Na hii inamfanya binti yangu kuwa na tabia ya kujiamini kuwa anaweza kufanya chochote kwa kuwa nawajenga kuwa hivyo kuanzia watoto.

Mimi ninaweza labda kwa sababu niliishi nje ya nchi lakini natamani wakina baba wengine wa Tanzania waige tabia hiyo ya kuwa sehemu ya malezi nyumbani.

Image caption Baba bora Tanzania,George Daniel na watoto wake

George Daniel ni mlinzi mwenye watoto wanne,anasema alikuwa mlevi sana wakati alipokuwa hajaoa lakini tangu amekuwa baba maisha yote ya starehe ameyaacha na yeye wakati wa mchana ndio anawajibika katika kuwalea watoto.

Watoto ni furaha katika maisha yake na anajivunia kuwa baba anayewajibika.

Lakini hata hivyo huenda kampeni hiyo ikahitaji jitihada,kwani wapo baadhi ya wanaume ambao bado wanaona jambo hilo ni kujidharirisha.

Emmanuel Temu,anasema majukumu yake ni kutoa fedha za matumizi hivyo mama ndio anapaswa kutimiza majukumu yake kwa kuwa hawezi kutafuta fedha za matumizi na wakati huohuo akae nyumbani kulea watoto.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii