Trump kuiongezea China ushuru wa forodha

China ni mteja mkubwa wa nguruwe kutoka Marekani
Image caption China ni mteja mkubwa wa nguruwe kutoka Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza mpango wa ongezeko la ushuru wa forodha kwa bidhaa za China, hali inayotarajiwa kuongeza vita vikali vya kibiashara kati ya nchi hizo mbili kubwa kiuchumi duniani.

Ametia saini hati ya maelekezo kwa maofisa juu ya namna ya kushughulikia suala la ushuru kwa bidhaa za mabilioni ya dola zinazoingizwa kutoka nchini China.

Trump amesema awali aliiona China kama rafiki, lakini amebaini kuwa vikwazo vinahitajika baada ya kugundua kuwa China inaonekana kutaka kujinufaisha kijanja katika uendeshaji biashara ambao umekuwa ukiingizia Marekani hasara ya mabilioni ya dola kila mwaka.

Amesisitiza kuwa China ni moja kati ya mataifa anayokusudia kuingia katika majadiliano ya kibiashara.

"Ndiyo tumeanza majadiliano na umoja wa Ulaya, kwa sababu wametuwekea vikwazo, kuna mazingira ambayo yanawaruhusu kufanya biashara na sisi."

"Lakini sisi hatuwezi kufanya biashara na wao. Wana vikwazo vikubwa dhidi yetu, wana ushuru wa forodha mkubwa sisi hatuna, siyo haki.Nao NAFTA wamekuwa wabaya kwetu, lakini tutajitahidi kurekebishana ama kufanya kitu cha ziada.

"Mpango wa kibiashara na Korea Kusini ni wa upande mmoja, unatakiwa kufanyiwa mabadiliko. Kwa hiyo kuna mambo mengi yanayotokea, lakini kwa suala la Uchina tutatumia kifungu 301 ambacho kitahusisha dola billion 60 ambazo ni sehemu tu ya hiki tunachokizungumza," alisema Bw Trump.

Hatua hii ya rais Trump dhidi ya China imekuja kufuatia uchunguzi wa mwezi Agosti kuhusiana suala la forodha ambao uliagizwa kufanyika na Trump mwenyewe.

China kwa upande wake imeonya na kuongeza kuwa iko tayari kujibu mashambulizi ya kibiashara dhidi ya Marekani na imeituhumu Marekani kwa kukiuka sheria za kimataifa za kibiashara.