Fahamu walimbwende watatu kutoka Tanzania waliobadilika kuwa wanaharakati

  • Esther Namuhisa
  • BBC Swahili
Maelezo ya picha,

Mashindano ya ulimbwende ni mlango wa fursa

Miss Tanzania wa zamani waiambia BBC namna ulimbwende ulivyofungua milango ya fursa za kibiashara na huduma kwa jamii.

Nancy Sumari

Anafahamika zaidi kama Miss Tanzania na Miss World Africa wa mwaka 2005, lakini leo hii mlimbwende huyu ni mjasiriamali na mwanaharakati wa kijami aliyeamua kuwainua vijana na wanawake zaidi katika nyanja mbalimbali za kijami.

Maelezo ya picha,

Miss Tanzania ,2005

Nancy Sumari, ni mfanyabiashara ambaye anamiliki kampuni ya habari kwa njia ya mtandao iitwayo 'bongo5'. Anasema mtandao huu wa habari unalenga kumjenga kijana kimawazo ili aweze kufanya maamuzi sahihi kwa kumpa habari na burudani.

Mbali na kampuni hiyo anamiliki pia taasisi ya mafunzo ya tehama kwa watoto inayochapisha mfululizo wa vitabu viitwavyo Nyota .

Shughuli hizi anazozifanya anasema zinampa fursa ya kujihusisha zaidi na miradi ya kuwawezesha wanawake, kutoa mafunzo kwa vijana na kusaidia katika kuboresha elimu nchini.

Maelezo ya picha,

Nancy Sumari akizindua kitabu chake cha hadithi na mashairi kwa watoto

Taji la ulimbwende kwa Sumari, ni jambo ambalo anajivunia sana kwa sababu limempa fursa ya kukutana na watu mbalimbali kutoka mataifa mbalimbali duniani na vilevile kutembea maeneo mengi duniani.

Anasema mashindano ya Miss Tanzania, ni jukwaa zuri ambalo linamjenga mtu kwa kile ambacho amelenga kukipata ingawa huwa inategemea na mtu mwenyewe na nini anataka kufanikisha.

Nancy anaamini kwamba sio kila kitu ambacho unaweza kukiona kwenye mtandao ndio uhalisia, kuna kazi kubwa nyuma ya pazia.

Mwaka 2017, Sumari aliweza kupata tuzo la vijana 100 wenye ushawishi zaidi Afrika, lifahamikalo kama 'Africa Youth Awards'.

Yeye pia ni mjumbe wa World Economic Forum, Mandela Washington Fellow.

Maelezo ya picha,

Baadhi ya wajasiriamali waliowahi kuvikwa taji la Miss Tanzania

Mbali na Nancy wapo walimbwende wengine walioenda mbali zaidi na kujivika mataji ya ujasiriamali na kujihusisha na shughuli zingine za kijamii.

Nasreen Karim

Maelezo ya picha,

Nasreen Karim,Miss Tanzania 2008

Nasreen Karim, alikuwa miss Tanzania mwaka 2008. Kwa sasa yeye ni mjasiriamali na mkurugenzi wa asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Enjipai Masai women foundation, inayoshughulika na kazi za utamaduni na sanaa ambazo anawashirikisha akina mama wa kimasai.

Biashara anayofanya alianza mara tu baada ya kumaliza muda wake wa Miss Tanzania.

Aliamua kuanzisha biashara hii kwa madhumuni ya kuwainua akina mama ambao wanajishughulisha na ubunifu wa shanga kwa kutengeneza vitu mbalimbali vya urembo .

"Nilipata wazo hili wakati nikiwa miss Tanzania, na liliweza kunipa fursa nzuri ya kushinda tuzo ijulikanayo kama 'Beauty with purpose' 'jambo ambalo niliona ni muhimu kuliendeleza."

Nasreen anasema kwa mwaka mmoja ambao alikuwa karibu na jamii akiwa miss Tanzania kulimuwezesha kugundua kwamba kuna umuhimu wa kuendelea kuwa karibu na jamii.

Katika hiki anachokifanya leo, anaona kama sehemu ya muendelezo wa pale alipoishia wakati akiwa miss Tanzania. Anasema anajivunia kwamba shughuli zake za kijamii anazozifanya sasa ndio zinazomtambulisha zaidi .

Maelezo ya picha,

Mjasiriamali wa bidhaa za utamaduni,Miss Tanzania 2008

Nasreen anaamini kwamba mashindano ya ulimbwende ni fani kama fani nyingine na inampa mtu muda mfupi sana wa mwaka mmoja ambao kama mtu ana malengo atafanikiwa kwa sababu ya jukwaa kubwa kutoka kwa vyombo vya habari na makampuni mengi yanayotaka kumtumia kwenye matangazo na kumuunganisha kwa watu wengi duniani.

Anasema hivi sasa shanga za kimasai ni bidhaa ambayo ina wateja wengi duniani kote na ina mvuto wa kisasa.

Brigette Alfred

Maelezo ya picha,

Miss Tanzania 2012,amejikita katika kuwawezesha watu wenye ualbino

Brigitte Alfred, msichana mwenye umri wa miaka 23, alipata taji la ulimbwende wa Tanzania mwaka 2012 akiwa na miaka 18.

Yeye amemaliza chuo kikuu mwaka jana, ambapo alikuwa anasomea Uchumi na masoko. Vile vile ni mkurugenzi wa asasi isiyokuwa ya kiserikali inayoitwa 'Empowering margnalised group' inayosaidia watu wenye ualbino nchini Tanzania.

Brigitte alipata nafasi ya miss Tanzania kipindi ambacho nchi ilikuwa ina janga kubwa la kujeruhiwa na hata kuuwawa kwa watu wenye ualbino hivyo shughuli nyingi za taji lake zilimuhamasisha yeye kuwa karibu zaidi na jamii hiyo.

Shughuli hizo pia zilimpa fursa ya kuwa mshindi wa tatu katika kipengele cha 'Beauty with Purpose' katika mashindano ya dunia.

"Jukwaa hili la Miss Tanzania lilinipa fursa ya kujionea na kujua ni nini kinakosekana katika jamii yangu, sina uwezo mkubwa sana lakini kwa kidogo nilichonacho ninajivunia kuwa nimemuwezesha kijana mwenye ualbino kuweza kulala katika nyumba salama baada ya kuwajengea bweni la watoto 300 huko shinyanga"

Brigitte anaamini kuwa kama asingekuwa Miss Tanzania basi asingeweza kuwa na maono mazuri kama haya, anasema hakuna ambaye aliyemshawishi kufanya chochote ila nafasi hiyo ilimpa fursa ya kufikia hicho anachokifanya.

Lakini vile vile anajivunia kupitia kampuni yake anaweza kumpa mafunzo kijana mwenye ualbino ambaye hajawahi kwenda shule kuweza kujua namna ya kutunza fedha katika akaunti, kujiajiri, kufanya biashara ndogo ndogo na kuanzisha vikundi vya kukopeshana na kujua namna ya kujikimu kimaisha.

Maelezo ya picha,

Miss Tanzania 2008,Brigitte Alfred

Wasichana wengi wanapata taji la miss Tanzania wakiwa na umri mdogo na ni wakati ambao unaweza kujijenga au ukapotea, anasema Brigitte.

Hata hivyo anaonya kwamba kama mtu hana watu wa karibu wa kumuunga mkongo ni ngumu kufanikiwa na kutumia fursa iliyopo mbele yao.