Thamani ya Sanaa ya uchoraji Tanzania

Brian anachora kwa kutumia kalamu ya wino Haki miliki ya picha Brian Rugangira
Image caption Brian anachora kwa kutumia kalamu ya wino

Picha hii ni ya Brian Rugangira ambaye uchoraji kwake ni kitu ambacho anakipenda tu na si ajira au kazi inayompatia kipato kama ilivyokuwa kwa wengine.

Brian ambaye makazi yake ni Mbeya ,nyanda za juu kusini mwa Tanzania anasema kuwa hakuwa anaona thamani ya uchoraji wake kuwa ni jambo ambalo linaweza kumpatia fedha.

Awali alikuwa anachora na kuzipanga picha zake nyumbani kwake tu lakini sasa ameanza kuziweka mtandaoni,jambo ambalo lilimshangaza sana kwa jinsi watu wengi walivyopenda picha hizo licha ya kuwa soko halioni haswa katika mazingira yanayomzunguka .

"Natamani sana sanaa yetu iongezeke thamani ,watu wawe na muamko,nadhani wadau wa sanaa wanaweza kusaidia sana katika jambo hili kwanza kwa kuanza kusambaza picha ambazo tunazichora maana zina ujumbe tofauti na picha za ajabu zinazosambaa mitandaoni ilimradi tu waandike ni nani aliyechora" Brian anasema.

Haki miliki ya picha Brian Rugangira
Image caption Brian Rugangira

'Wanapenda kuchorwa wao wenyewe'

Sanaa ya ufundi ambayo inajumuisha uchoraji, upakaji rangi picha, uchongaji na utengenezaji wa mapambo mbalimbali ya asili ni utamaduni ambao ulianza nchini Tanzania takribani miaka 5000 iliyopita,sanaa hii ilianza nchini Tanzania katika michoro ya mapango ya Kondoa Irangi.

Kwa miongo kadhaa, Tanzania imejulikana kwa umahiri wa uchoraji wa picha licha ya kuwa Watanzania wenyewe wametajwa kujiona kuwa sio walengwa husika.

Picha za Tingatinga ni miongoni mwa sanaa maarufu sana nchini humo, tangu miaka ya sabini na kadri muda unavyozidi,ubunifu wa picha pia unakua kila kukicha.

Pamoja na utajiri mkubwa wa kihistoria katika upande wa utengenezaji na uuzaji wa picha hizi, bado thamani ya sanaa hiyo ya uchoraji ina muamko hafifu kutoka kwa wazawa.

Image caption Masoud Kibwana anasema Watanzania wanapenda picha zinazowaonesha wao

Masoud Kibwana ni mchoraji wa kutumia rangi mbalimbali ,yeye anasema picha zake zimewalenga watu wote,wageni na wenyeji lakini anasema asilimia kubwa ya wateja wake ni wageni.

Masoud anadhani hii ni kutokana na mtazamo wa muda mrefu wa baadhi ya wazawa kwamba michoro ni kwa ajili ya wazungu.

Wengine husema gharama ni kikwazo kinachowafanya watanzania wengi wasinunue bidhaa zao lakini anashangaa kwamba wapo Watanzania ambao huwa wananunua picha iliyotengenezwa China kwa gharama kubwa zaidi.

Huwezi kusikiliza tena
Masanja mchoraji ametupilia mbali penseli na rangi katika uchoraji na kuhamia kwenye moto

Na hali hii inapelekea wasanii wengi katika fani hiyo kuamua kuchora vitu ambavyo vinawavutia watalii kwa kuwa wao watanunua kwa bei nzuri na soko kuendelea kuwalenga wao zaidi, Masoud aliongeza

"Nadhani kwamba picha tunazozichora Watanzania hawazipendi ,kwa kuwa wengi wetu tunachora picha za asili yetu mfano kama picha za wamasai,nyumba za zamani na yani picha zile zinazomuwakilisha muafrika na wao wanapenda picha za mtazamo tofauti".

Image caption Picha aliyechora Masoud Kibwana

Masoud anasema kwa utafiti aliofanya amegundua kuwa Watanzania wanapenda picha ambazo zinaonesha uhalisia wa kitu fulani cha sasa.

Mfano sasa hivi wengi wanapenda kuchorwa wao wenyewe au ndugu zao wa karibu lakini sio kununua picha cha kufikirika ambazo zinatengenezwa na wasanii wengi.

"Ila kwa ujumla pia hii ni tabia tu iliyojijenga kwa Watanzania wenyewe, hata ukiwalinganisha na nchi za Afrika mashariki, kwa mfano sisi tunakuwa na maonyesho mengi ya picha ambayo ni bure kabisa lakini onyesho hilo nikilifanyia Kenya,watu asilimia 75 watakuwa ni wenyeji na wageni ni asilimia ishirini na tano."

"Hii ni tofauti na Tanzania ambapo asilimia 75 ni wageni na asilimia 25 ni wenyeji tena unaweza kukuta ni wasanii wenzako wamekuja kukuunga mkono" anasema Masoud.

Image caption Je,ni kweli sanaa ya uchoraji inayofanywa na Watanzania haipendwi na wenyeji?

'Utamaduni wa kununua picha'

Aidha si wasanii wote ambao wanaona kuwa sanaa ya uchoraji inayofanywa na Watanzania haipendwi na wenyeji.

Gadi Ramadhani yeye ni mchoraji wa mambo mbalimbali ya kijamii akiwakilisha taswira ya jamii husika kulingana na nyakati usika,mfano huwa anachora michoro inayowakilisha unyanyasaji wa kijinsia,ndoa za utotoni na hata siasa kwa sababu yote hayo ni maisha ya Mtanzania.

Haki miliki ya picha GADI RAMADHANI
Image caption Gadi anatumia michoro kuzungumzia mambo mbalimbali ya kijamii

Gadi anaamini kwamba sanaa ya uchoraji ni lugha ambayo ina ulingo mpana na kila msanii ana lugha yake na wapo wasanii ambao wanafanana katika mfumo wa sanaa wanayofanya na wengine hawafanani kabisa.

Ni sawa na msanii wa muziki anakuwa na washabiki ambao wanapenda aina ya muziki mfano, anayependa reggae anaweza asiwe mpenzi wa taarab kwa mfano, basi hata kwenye picha wapo mashabiki ambao wanapenda rangi ,muonekano wa picha au mada inayowakilishwa kwenye picha.

Haki miliki ya picha GADI RAMADHANI
Image caption Watanzania wachache wanaenda kuangalia maonesho ya wachoraji wazawa

'Angalia soko linataka nini'

Utamaduni wa kununua picha na kuangalia ni utamaduni wa Ulaya ,sisi ni nafasi ya maisha inayotupa kipato na tunathamini mchango wa Watanzania katika kazi zetu hata kama ni mdogo ila ndio viongozi na utawala kwa ujumla waanze kutoa muamko kwa jamii .

Kwa upande wake mtaalamu wa sanaa nchini Tanzania, Dk.Vicensia Shule, anasema sio kwamba Watanzania hawathamini sanaa ya uchoraji nchini Tanzania.

Lakini anaona kuwa lazima wasanii wenyewe lazima wabadilike ili Watanzania waone umuhimu wa sanaa tulionayo.

"Sanaa ya uchoraji sio chakula,sio malazi lakini inaweza kumletea malazi na chakula kwa mchojari,hivyo wasanii wana ulazima wa kutafuta namna ya kuweka sanaa hii iwe na umuhimu kwa maisha ya mtanzania kwa kuwa kabla mtu hajanunua picha lazima awe amejitosheleza katika mahitaji muhimu kama matibabu na chakula.." Dk. Shule aeleza.

Dk. Shule anasema kuna ulazima wa wasanii wa Tanzania wabadilike kwanza kwenye upande wa suala la gharama,bei zao ziko juu sana.

Image caption Dk Vicensia anasema wachoraji wazawa wanaweka bei kubwa katika kazi zao kuliko uwezo wa Watanzania

Mtanzania wa kipato cha kawaida tena sio cha chini ni vigumu kununua picha ya laki saba mpaka milioni.

Njia nyingine ya kubadilika ambayo Dk. Shule ametaja ni kuhusu mawazo wanayotumia katika uchoraji,wanatumia hisia zaidi badala ya kuangalia soko la Tanzania linataka nini.

Kama soko linataka picha za Masai,Tingatinga au Wamakonde basi ndio hizo wazilenge.

Lakini vile vile wanabidi wafahamu wamemlenga nani,ni wazi kuwa sanaa ya uchoraji inayomvutia mtalii haiwezi kumvutia Mtanzania,hivyo utafiti unahitajika zaidi.

'Watanzania wengi wanaona aibu kujikubali'

Hata hivyo sio tu kwenye upande wa uchoraji ndio kuna changamoto katika mapokeo ya Sanaa ,Jopton Makeke ni mbunifu wa masalia ya mimea na wanyama, hivyo huwa anatengeneza mavazi ya asili pamoja na maonyesho ya picha hizo za asili.

Haki miliki ya picha MEKEKE
Image caption Makeke anatengeneza mavazi ya asili pamoja na maonyesho ya picha hizo za asili.

Yeye anasema kwamba ni miaka sita sasa tangu aanze kufanya kazi hii ya ubunifu wa taswira ya muafrika, lakini bado changamoto ni nyingi.

Katika kupokelewa kwa kazi yake anadhani kwamba kama angekuwa anabuni mavazi ya kisasa basi angekuwa mbali.

Wengi wana mtazamo kuwa sanaa anayofanya ni ushamba au kutokwenda na wakati na Watanzania wengi wanaona aibu kujikubali wao ni kina nani na asili yao ni wapi,mtazamo wa wengi ni kutaka kwenda na usasa, dhana ambayo inarudisha jitihada zao nyuma kama wasanii.

Aidha kuna sanaa ambazo hata mimi mwenyewe nilishuhudia licha ya kuongea na baadhi ya Watanzania na kupata majibu yanayofanana kutoka kwa wengi kuwa hizo ni bidhaa za watalii.

Picha hiyo inaonyesha vitu mbalimbali kama kiti,viatu, kofia na mapambo mbalimbali ya nyumbani,hivyo vyote vimetengenezwa na chua za plastiki pamoja na makopo.

Alphonce Saidi ndio mbunifu sanaa hii ambapo anasema kiatu kimoja kina gharama ya shilingi laki moja mpaka laki moja na nusu.