Waathirika wakubwa ni wanawake na watoto

Mvua za masika ya mwezi aprili
Image caption Mvua za masika ya mwezi aprili,2018 zimesababisha vifo vya watu 14 jijini Dar es salaam

Mvua inaponyesha katika maeneo ya mashambani huwa ni baraka na hata wengine hufanya matambiko maalumu ili mvua inyeshe, jambo ambalo ni tofauti katika maeneo ya mijini.

Mvua kubwa inaponyesha jijini Dar es Salaaam, vyombo vya habari hutaarifu juu ya vifo vilivyotokea, adha ya usafiri na umeme.

Mjadala mkubwa huwa kuhusu uzembe wa watu kuchagua kuishi maeneo ya bondeni.

Image caption Serikali ya Tanzania imewataka wakazi wa mabondeni kuhama eneo hilo mara kwa mara bara

Eneo ambalo linaathirika zaidi na mvua katika jiji hili kubwa la biashara la Dar es Salaam, nchini Tanzania liko maeneo ya mjini ambapo wengi wanadai kulazimisha kuendelea kuishi hapo kutokana na unafuu wa maisha.

Pamoja na tahadhari zinazotolewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa na mamlaka mbalimbali, Serikali ya nchi hiyo imewahi kufanya juhudi mara kadhaa kuwahamisha watu hao kutoka katika maeneo ya mabondeni lakini inawezekana hawakuhamishwa wote au wengine walikataa au walivyoondolewa walirejea tena katika maeneo hayo.

Ni miaka saba sasa tangu serikali ya Tanzania ilipotoa eneo kubwa kwa ajili ya wakazi wa mabondeni ili kuepusha maafa ya mvua za Elnino mwaka 2011 huko Mwabwepande.

Mwaka 2015 nilibahatika kufanya taarifa juu ya wakazi hao kuhama na wengi niliowakuta katika maeneo hayo ya mabondeni walidai ugumu wa maisha ya eneo waliopewa inawalazimu waendelee kuishi hapo.

Wiki hii watu 14 wamepoteza maisha jijini humo kutokana na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko.

Image caption Shule zote jijini Dar es salaam zilifungwa kwa muda wa siku mbili

Kama ilivyo kwenye tafiti nyingi duniani, wanawake wamekuwa wahanga wakubwa wa madhara ya mafuriko na mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo mbalimbali duniani.

Licha ya lawama nyingi zinazotolewa kwa wakazi hao wanaoishi mabondeni nchini humo inawezekana pia sio wote walioweza kufikiwa au wana mbadala wa maisha wanayoisha.

Image caption Wakazi wa mabondeni wakiokota masalio ya vitu vyao mara baada ya mvua kubwa kunyesha

Katika eneo hili la Kigogo, jijini Dar es Salaam nilikuta msiba wa mwanamke mjamzito aliyekufa kutokana na kuangukiwa na ukuta wa nyumba yake baada ya mvua kubwa kunyesha.

Lakini pia nilikutana na wanawake wengi na simulizi za maisha yao zikionekana kufanana, wengi wao ni wajane, wazee na wanawake wanaowalea watoto pekee yao.

Image caption Wanawake hawa wajane walalamikia adha ya mafuriko na uwezo wao wa kimaisha

Hawa wote wameishi katika maeneo hayo kwa miongo kadhaa na wanatambuliwa na serikali kwamba ni wananchi wanaoishi maisha duni ambapo wanapokea msaada wa fedha za wananchi wa kaya za chini wa mfuko wa Tasaf.

Isabella Leonard mwenye umri wa miaka 60, ni mjane ambaye anaishi maeneo ya bondeni tangu mwaka 1997.Mume wake alifariki na kumuachia chumba kimoja pamoja na mtoto mmoja ambaye pia alifariki mwaka 2015.

Bibi huyo anaendesha maisha yake kwa kutegemea kupokea fedha kutoka mfuko wa Tasaf ambapo anapokea kiasi cha shilingi elfu 30 kila baada ya miezi miwili lakini fedha hizo hazikidhi kulea wajukuu watano.(Tasaf ni fedha zinazotolewa kwa kaya maskini nchini Tanzania).

.

Image caption Anasema ni maumivu makali ambayo anayapata kutokana na maisha anayoishi kwa miaka yote hiyo na hakuwahi kupata msaada wowote wa kutakiwa kuhama

Bi. Isabel aliongeza pia kwa kusema kuwa bora kanisa huwa wanapata msaada kidogo.

"Tunateseka sana, umri umeenda, sina kaka, sina mume, dada yangu mzee zaidi na wote maisha yetu shida. Wengi tunakimbilia Parokia ya Msimbazi maana ndio wanatusaidia kidogo lakini hatuna msaada wowote tunaopata kutoka serikalini, na sasa hata shule tumekatazwa kulala huko hivyo ni baadhi ya majirani tu ndio wanasaidia wengine hawajali".

Image caption Makazi ya bondeni,Dar es salaam

Lakini vilevile bibi huyo ambaye nyumba yake iko bondeni kabisa na ilikuwa ya mwisho wa ukingo wa mto msimbazi tangu miaka ya tisini, yeye pamoja wananchi wengine wa eneo hilo wanadai kuwa hali ya sasa ya mafuriko imekuwa mbaya zaidi tofauti na miaka iliyopita.

Image caption Ukingo unaodaiwa kusababisha madhara zaidi ya mafuriko,katika eneo la kigogo Dar es salaam

Kina mama hao wamedai kuwa siku hizi mafuriko yamezidi na yanaanza muda ya saa 9 usiku wakiwa wamelala, kuogelea hawajui ila wanabaki kutambaa tu na huwa ni hekaheka.

Hali ya eneo hilo ni la kuhama hama tu usiku mvua ikinyesha wanahamia kwa majirani na ikitulia wanarudi kufanya usafi, wanasema maisha yao kutwa ni ya wasiwasi.

Bi. Beatha Kasiani mwenye umri wa miaka 72, anasema mafuriko makubwa kabisa ambayo hawezi kuyasahau yalikuwa 2011. Anaishi na wajukuu wake wote na watoto sita wa kike, ambao wengine waliachwa na waume zao na mwingine alifiwa na mumewe.

Image caption Umaskini ndio chanzo cha wao kukosa eneo la kuishi zaidi ya mabondeni

Huku bi. Evarista anasema maisha yao yanazidi kuwa katika hofu pindi wanaposikia nyumba kadhaa zimebomolewa na mvua katika maeneo ya jirani kama vile Vingunguti.

"Hakuna mtu anaependa kuteseka, haya ni mazingira magumu mno tunaomba serikali itusaidie maana sisi wenyewe hatuwezi na hatuna mbadala."

Wanawake hawa wanadai kuwa wanapata tahadhari ila sehemu ya kwenda ndio hawana. Wanaendelea kusema kuwa, maisha yao ni ya kupanda na kushuka huku kila mwaka wakilazimika kununua magodoro kwa sababu yakishalowa hayawezi kutumika tena.

Aidha, Afisa Mtendaji wa eneo hilo, Barama Kaiza anaamini kwamba watu hao wa mabondeni wameshazoea hali hiyo maana sio mara ya kwanza kutokea. Ni eneo ambalo limekua likiathirika kwa muda mrefu.

Ingawa kwa upande wao kama serikali wamekuwa wakishirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo Benki ya Dunia, kufanya utafiti na tathmini ya namna ya kutatua tatizo hilo. Pila kuna miradi mengine inayoendelea ya kutatua tatizo hilo.

Maelezo kutoka viongozi wa maeneo hayo ya bondeni yanafanana

  • Changamoto ni ugumu wa wananchi kuhama kwenda maeneo mengine. Tahadhari huwa zinatolewa ila nahisi wamezoea.
  • Serikali haina uwezo wa kuwafidia walichopoteza, ingawa mara nyingi inajitahidi kuwaepusha maafa.
  • Kuna ambao walichukua maeneo ya msaada lakini bado wanaishi hapa kwa sababu ni karibu na mjini.

Huko Vingunguti na Msimbazi kilio ni kile kile kuwa wanataabika na hali hiyo ya mvua na kumbukumbu za mwaka 2011 zinarejea kwa wengi, wanasema maisha yao ni ya kukaa chonjo.

Wengi wa wakazi hao wamekana kupewa msaada wa viwanja kama serikali inavyodai.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa nchi hiyo Khassim Majaliwa ametoa wito kwa wakazi wa mabondeni kuhama maeneo hayo na kusema mvua bado zinaendelea na serikali inakamilisha mipango ya kurekebisha miundo mbinu ya maeneo hayo ya mabondeni.

Wakazi wa Mwabwepande;Eneo lililotengwa na serikali ya Tanzania kwa ajili ya makazi ya wahanga wa mafuriko

Image caption Baadhi ya nyumba za maeneo ya Mwabwepande zinaonekana ni za kifahari na kuwapa wasiwasi wengine kuwa yawezekana wahanga hawakuhamia

Kwenye makazi haya ambayo wahanga wa mafuriko walikabidhiwa ni kweli kuna nyumba za watu wa uwezo wa hali ya juu na watu wa hali ya chini au wastani.

Bi.Theresia ambaye ni mmoja wa wajumbe wa eneo hilo anasema kwamba kuna baadhi ya wahanga waligoma kuhamia huko kwa kudai kuwa ni porini na waliohamia walipewa jina la wahanga wa porini hivyo huko kuna waliouza na kuna maeneo yasiyoendelezwa mpaka sasa na hawajulikani walipo.

Image caption Wakazi wa hapa wanasema walianza kukaa kwenye mabati na sasa wana nyumba ,wanafurahia maisha kwa sasa

Katika makazi haya, walihamia mwaka 2014, wanasema wanashukuru Mungu kwa kuwa adha ya maji tena hakuna, maana roho zilikuwa juu juu pindi wanapoona mawingu.

Mwanzoni iliwawia vigumu hata wao maana walipewa viwanja tu, ndio maana walianza kwa kujenga mabanda na baadae wakaweza kujenga na hiyo ndio sababu ya wengi kushindwa kuhamia huko.

Walivyohamia kulikuwa hamna maduka wala huduma muhimu za kijamii lakini sasa hivi, wao wenyewe wamefungua maduka, hivyo wanashukuru kuna hospitali, umeme, kituo cha polisi ingawa wanasema, changamoto iliyopo hivi sasa ni barabara.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii