Bodi ya Filamu Kenya yapiga marufuku filamu ya wapenzi wa jinsia moja

Maudhui ya filamu hiyo yanahusisha mapenzi ya jinsia moja
Maelezo ya picha,

Maudhui ya filamu hiyo yanahusu mapenzi ya jinsia moja

Bodi la Filamu la Kenya (KFCB) imeipiga marufuku filamu iitwayo 'Rafiki' inayogusia masuala ya mapenzi ya jinsia moja.

Filamu hiyo ni ya kwanza kutoka Kenya kuchaguliwa ili kuonyeshwa katika tamasha la kimataifa la Cannes mwaka huu.

Tamasha la Cannes, ni miongoni mwa matamasha ya filamu makubwa duniani ikiwa pamoja na tamasha la Oscars. Wanafilamu,watayarishaji na waongozaji wa filamu wanakutana sio tu kushindanisha filamu lakini pia ni nafasi kubwa ya kuuza filamu zao kwa makampuni makubwa.

KFCB imepiga marufuku filamu hiyo kuonyeshwa hadharani au kutangazwa kwenye televisheni na kusambazwa, ikisema maudhui ya filamu hiyo inayoonesha mapenzi ya jinsia moja kati ya wanawake wawili, inakiuka sheria za Kenya.

Filamu hiyo imeandikwa na kuongzwa na Wanuri Kahiu aliyetangaza habari hizo za kupigwa marufuku kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, akisema "niliamini kuwa watu wazima Kenya wamenyimwa haki zao za kujichagulia maudhui wanayoyataka kuyaona"

Ruka Twitter ujumbe, 1

Mwisho wa Twitter ujumbe, 1

Hadithi ya Rafiki ni kuhusu wasichana wawili Kena na Ziki, marafiki wa karibu ambao baadae walikuwa wapenzi. Familia zao wako katika pande tofauti za kisiasa.

Wanakutana na shinikizo kubwa ambalo linaathiri urafiki wao. Hali hii inawafanya kufanya maamuzi magumu baina ya furaha yao au usalama wao.

KFCCB inasema kuwa " baadhi ya picha zinazoonyesha mapenzi ya jinsia moja zinakiuka sheria, utamaduni na maadili ya Wakenya. Inajaribu kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja kati ya wanawake"

Bodi hiyo imeonya kuwa mtu yeyote atayekutwa na filamu hiyo atachukuliwa hatua za kisheria.

Wanaharakati wanaotetea mapenzi ya jinsia moja waliandika kwenye mtandao wa Twitter wakishutumu bodi hiyo .

Ruka Twitter ujumbe, 2

Mwisho wa Twitter ujumbe, 2

Mwezi Juni mwaka uliopita, bodi hiyo ilipiga marufuku baadhi ya vipindi vya televisheni katika ving'amuzi vya DSTV na GOTV vilivyosemekana kuunga mkono mapenzi ya jinsia moja.

Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja ni kinyume ya sheria kama nchi nyingi barani Afrika. Tendo la ngono kati ya watu wa jinsia moja inahukumu ya miaka 14 gerezani nchini Kenya.

Mwezi uliopita, mahakama ya Kenya iliamua kwamba kitendo cha kuwalazamisha kuwapima kwa nguvu sehemu za siri za wanaume ilikubaini kama wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja, ni kinyume cha sheria .