Wakati au Jamii? Ipi yafaa kuwa sababu sahihi ya kupata mwenza

Jamii inachangia kuongeza msukumo wa mabinti kutaka kuolewa Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jamii inachangia kuongeza msukumo wa mabinti kutaka kuolewa

Majira ya saa nane mchana siku ya Jumapili mvua kubwa ikiwa inanyesha, bila shaka wengi watakuwa wametoka kanisani na kupumzika nyumbani .

Lakini si kwa mamia ya wasichana ambao wamejumuika kwa pamoja katikati ya jiji la Dar es salaam katika ukumbi wa Makumbusho.

Wengi wakiwa wameinua mikono yao juu, mchanganyiko wa sauti za vilio na nyimbo, ulikuwa umetawala maombi ya hisia.

Image caption Colle Karyn akiwahuburia wasichana ambao bado hawajaoelewa

Jukwaani alikuwepo Colle Karyn.

Wasichana wote wakiitikia kwa kuimba Amen.

Karyn alikuwa akiongoza kongamano la ' Grace for singles', kongamano maalum kwa ajili ya wasichana ambao hawajaolewa.

Bi. Karyn, ambaye anajitambulisha kuwa mtumishi wa Mungu, anasema aliwiwa kuanzisha makongamano ya aina hii kwa ajili ya wasichana wasioolewa tu baada ya kuona kuwa watu zaidi ya asilimia 80 waliokuwa wanakuja kwake kwa ajili ya kutafuta msaada wa kiroho, walikuwa wakimuelezaa juu ya changamoto au matatizo katika ndoa zao.

"Niliona ni bora kuwawahi wale ambao hawajaingia kwenye ndoa, kwa kuwapa elimu waweze kuwa wamejiandaa na maisha watakayoyakuta katika ndoa."

Huwezi kusikiliza tena
Wanamuziki wakabili unyanyasaji katika ndoa Kenya kupitia muziki

Mwanzoni, Bi Karyn anasema, wazo hili la 'Grace for single ladies' lilikuwa likiwalenga vijana kwenye mitandao ya kijamii pekee.

Anasema vijana wengi wamekuwa wakitamanishwa kuingia katika ndoa kutoka na picha za kuvutia za harusi na taarifa za ndugu ama rafiki zao ambao aidha wameoa au kuolewa au wanatarajia kufanya hivyo.

Picha za harusi za kifahari na kupendeza zinawapa motisha wasichana wengi hasa waishio mjini, kufanya bidii ili na wao waweze kufanya harusi kama waliyoiona katika picha.

Kwa upande mwingine pia, mitandao hiyo hiyo inawafanya vijana wengi kusumbuliwa na msongo wa mawazo juu ya hatma ya vijana hawa kuhusiana na kuoa au kuolewa.

Karyn anasema vijana wengine hata wamediriki kufanya vitu kwenye mitandao hiyo ambavyo ni kinyume na maadili kwa lengo tu la kuwinda kuoa au kuolewa na mwisho wa siku kuingia kwenye mahusiano ambayo si sahihi.

Haki miliki ya picha Colle Karyn
Image caption Baadhi ya wasichana wakiwa kwenye kongamano la wasichana wasioolewa

"Wengi wanaingia kwenye ndoa bila kujiandaa na matarajio yao yanakuwa hayajatimia ndio maana kuna changamoto kubwa katika ndoa" anaeleza Karyn .

Maria mwenye umri wa miaka 25 ni miongoni mwa wasichana waliohudhuria kongamano hilo,yeye anasema kongamano la kidini la namna hii linasaidia vijana katika maadili na anaamini kwamba neno la Mungu linasaidia kutoa mafundisho na kutoa muongozo wa maisha.

"Wasichana wengi wameanguka mara kadhaa katika mahusiano ya kimapenzi ambayo yanachukua sehemu kubwa sana ya maisha yao,

Mahusiano yanawafanya wengine kukata tamaa,wanashindwa kufanya kazi zao ,kutimiza ndoto zao na kuna ambao hata wanajiua kwa sababu ya kutendwa katika mahusiano au kuachwa na wapenzi wao".

Haki miliki ya picha Anointed_room
Image caption Mtumishi Karyn akitoa mahubiri

Wakati Happy Kamiliusi mwenye umri wa miaka 29, anaamini kwamba taasisi ya ndoa imepoteza heshima kwa kiwango kilichokuwepo zamani. Anasema hii ni kwa sababu hakuna mafunzo sahihi au misingi mizuri kwa vijana wengi kabla ya kuingia katika ndoa.

"Kongamano la namna hii linatukumbusha kuona thamani ya miili yetu na umuhimu wetu duniani hata kama hatujaolewa,sehemu kama hizo tunatua mizigo ya kuachwa, maumivu ya kutengwa, kupata moyo wa kusonga mbele na kutimiza ndoto zetu".Happy aeleza

Kwa upande wake Hellen Matata ,yeye anashukuru kwamba hajawahi kupata msukumo wowote kutoka kwenye familia yake ili aolewe ingawa anaona msukumo mkubwa wa kuolewa upo kwenye jamii,anaona wengine wakiacha shule kwa sababu hawajaolewa.

Huku wengine wanahisi maisha hayawezi kukamilika kama hawajafunga ndoa hata kama wana mafanikio makubwa ya elimu au kazi,wengine wanaona ni laana na kutokuwa na bahati katika maisha.

Aidha Hellen anaongeza kwa kusema wengine wanadhani kwamba jamii inaona thamani ya maisha ni ndoa na hawangaalii mafanikio mengine jambo ambalo anasema si sahihi na linawasononesha wengi.

"Mila na desturi za kiafrika inamtaka mwanamke avumilie, mwanamke ana mzigo mkubwa wa kubeba matatizo. Ndoa ni zaidi ya gauni ambalo mtu analivaa siku ya harusi." Anasema Hellen

Msukumo wa kutaka kuolewa kutoka kwa wasichana wenyewe na jamii.

• Umri huwa ni kigezo kikubwa sana na wengi wanapoona wale waliosoma nao wameolewa basi na wao wanataka kuingia kwenye ndoa.

• Wengi wanahisi wakifika miaka 25 hawajaolewa au hawana wachumba, basi wanakuwa na wasiwasi kwa nini hawajaolewa au hawana wachumba wa kuwaoa.

• Maswali mengi kutoka kwenye jamii zao ya kwamba unaolewa lini? Na akijiangalia ana miaka 32 na hajaolewa yanawafanya waishi maisha ya mashaka.

• Wengine wako tayari kufanya kila linalowezekana ili tu waolewe. Matokeo yake hujikuta katika mahusiano ambayo si sahihi.

Aidha idadi kubwa ya wasichana wasioolewa iliyojitokeza katika kongamano hilo la 'Grace for Single inadhihirisha wazi msukumo uliopo katika jamii juu ya ndoa na hofu iliyoko kwa wasichana wengi ambao wanataka kupata suluhu ya changamoto hiyo inayowakabili.

Mtumishi Karyn anasema wakati umefika ambapo wadada wanatakiwa kuacha kuangalia saa zao maana umri kuwa mkubwa sio kigezo cha mtu kutojiona kuwa yuko huru, haina haja ya kupata wasiwasi na umri au miaka inavyozidi kwenda.

Mtaalam wa Saikolojia kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam,Daniel Marando anasema jamii inakuwa ina matarajio mengi sana kwamba kama binti akimaliza masomo basi kinachofuata ni kuolewa.

Hivyo kama muda wa shule umepita na hamna mtu amekuja kutuma posa katika familia basi malalamiko na maswali kwa binti yanaanza kutoka kwa familia.

Wazazi mara nyingi wanakuwa hawajui mfumo wa maisha ya watoto wao na wanabakia kutojua sababu ya mabinti zao kutoolewa.

Hali hii inawapelekea mabinti hao kuchanganyikiwa na kuathirika kisaikolojia.

Image caption Umri muafaka kuolewa kwa mwanamke ni upi?Dada funguka kwa kutuma mtazamo wako kupitia swahilibbc@gmail.com

Je kuwepo kwa hali hii inamaanisha waoaji hawapo?

Mwanasaikolojia Marando anasema suala la kuolewa ni suala la muda,miaka 20 mpaka 25 huwa ni kipindi cha neema .Kipindi hiki waoaji huwa wanatokea lakini wasichana wengi wanakuwa na uchaguzi mwingi wa aina ya wanaume wanaotaka waolewe nao mara mwingine atasema nataka mwanaume mrefu,mara mwanaume anayefanya kazi fulani na sababu nyingine nyingi ambazo zinawafanya wakose msimamo.

Image caption Miaka 20 mpaka 25 ni umri ulio rahisi zaidi kuolewa

Wasichana hao wanapofika miaka 27,28,29 wanakuwa wanataka kuolewa tena bila kuwa na uchaguzi na kusahau kuwa kuna wengine ambao wako kwenye umri wa miaka 20,21 na wako tayari kuolewa pia

Suala la wanawake kutaka kuimarika kiuchumi ni changamoto ambayo inakuja kiasili tu kwa sababu wanaume wana tabia ya kutotaka kuoa wanawake waliowazidi uwezo katika maendeleo.Wanaamini kwamba kama wakioa wanawake wenye fedha zaidi yao basi watakuwa wanatawaliwa ndio maana ni ngumu kwa wanawake waliofanikiwa sana kuolewa.

Mfumo wa elimu pia unasababisha changamoto kwa wasichana wengi kutoolewa pia .Wanaume hawaangalii elimu kama kigezo cha kuoa,wanatafuta wanawake ambao wanaweza kuwanyenyekea na wapo wanaume ambao wanauoga kuoa mwanamke ambaye amesoma sana hivyo ni rahisi msichana aliyesoma kiwango cha diploma kuolewa kuliko mwenye shahada.

Kutokana na sababu hizo basi unakuta idadi kubwa ya wasichana wakifika miaka 32,wengine wanapata mawazo ya kuzaa hata na waume wa watu na kuwalea watoto wenyewe .

Hivyo kupelekea idadi ya 'single mothers' kuongezeka pia.

Lawama nyingine pia zinaenda kwa wazazi kushindwa kuwapa malezi bora watoto wao wa kike ,baadhi ya wanaume huwa wanaangalia ni majukumu gani mke wake mtarajiwa anaweza kuyafanya kama mama au kama mke.Familia nyingi zina tegemea wasaidizi kufanya kazi zote za nyumbani na watoto wa kike wanashindwa kufanya kazi yeyote ya nyumbani wenyewe.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii