Kinachowavutia wanawake wengi katika Ujasiriamali

Tamasha la wajasiriamali wanawake,Purple planet Haki miliki ya picha Purple Planet
Image caption Tamasha lililojumuisha wajasiriamali wanawake zaidi ya elfu mbili,Purple planet

Takwimu za usawa wa kijinsia katika ajira zinaonyesha kwamba kufikia mwaka wa 2014 Watanzania milioni 2.1 walikuwa wameajiriwa katika sekta rasmi , ikiwa ni pamoja na serekalini na sekta binafsi, kwa mujibu wa kituo cha taifa cha takwimu nchini humo

Hata hivyo takwimu rasmi za serikali zinaonyesha pia kwamba zaidi ya 60% ya wanawake walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 24 yaani million 13.9 wanajishughulisha na shughuli zisizo rasmi yaani biashara ndogondogo na kilimo.

Hii maana yake ni kwamba ni asilimia 0.75 tu ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi ndio wapo katika sekta rasmi. Kwa maneno mengine, idadi kubwa ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi nchini Tanzania ni wajasiriamali

Wanawake hawa wanajihusisha na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubuni bidhaa mbalimbali huku wengine wakifanya biashara katika vikundi au mtu mmoja mmoja.

Image caption Wanawake wajasiriamali nchini Tanzania

Awali waliitwa wafanyabiashara ndogondogo. Ukikutana na mama barabarani anauza mandazi au vitumbua atakuambia yeye ni mfanya biashara ndogondogo na thamani ya kile alichokuwa anakifanya kikawa kinaonekana kwa taswira ya udogo pia.

Lakini sasa wengi wao wamepiga hatua na kuzipa thamani bidhaa wanazouza na kutengeneza.

Katika tamasha la wanawake wajasiliamali wajulikanalo kama 'Purple planet' lililofanyika jijini Dar es Salaam, hivi karibuni, na kujumuisha wanawake zaidi ya elfu mbili kutoka nchini humo ili kuonyesha shughuli wanazozifanya.

Juliana Nyanda kutoka asasi hiyo anasema sasa ujasiriamali wa wanawake sio ule mdogo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwa sababu zamani unaweza kusema kuwa hawakupata fursa ya kupata elimu ndio maana waliingia kwenye ujasiriamali lakini sasa wajasiriamali wengi ni watu waliopata elimu nzuri pia.

Asasi hiyo isiyokuwa ya kiserikali ya Purple Planet inawawezesha wanawake kupitia mitandao na kuwapa mafunzo,ushauri na muongozo wa kufanya kile wanachopenda kukifanya na wanafanikiwa .

Biashara ni jina

Haki miliki ya picha Malkia wa viungo
Image caption Malkia wa viungo vya upishi,nchini Tanzania

Teddy Bernad ni mjasiliamali wa viungo vya chakula ambapo kutokana umahiri wa utengenezaji wa viungo hivyo, amepachikwa jina la Malkia wa viungo.

Yeye ni msomi wa saikolojia lakini sasa amejiajili na kujishughulisha na utengenezaji wa viungo vya chakula. Alianza kufanya biashara hii kutokana na shauku yake binafsi ya kupenda viungo.

"Nilikuwa na utundu tu wa kuchanganyachanganya viungo na kusoma kwenye mtandao na kuweka vyakula vyangu kwenye mitandao na maswali niliyokuwa napata ya namna nnavyotengeneza na nikiwaelekeza wanakuwa hawaelewi nikaona hapo kuna fursa na nikaamua kwenda kusomea masomo ya muda mfupi ya uzindikaji chakula ".

Malkia huyu wa viungo anasema anatumia malighafi ya asili kama magome ya miti,mbegu na majani kupata aina 24 ya viungo.

Licha ya ajira hiyo aliyoipata mjasilia mali huyu anafanya vipindi vya radio na televisheni katika kituo kimoja cha luninga nchini Tanzania.

"Watu wengi wamezoea kula chapati za kukanda tu na mafuta kawaida ila kuna chapati ambazo unaweza kupika ukachanganya mdalasini, hiriki, galam masala au kiungo kingine."

Ujasiriamali ni ubunifu wa kitu unachokipenda

Image caption Nice Kahaya,fundi cherahani ambaye ni mtangazaji wa radio

Nice Kahaya ambaye ni mtangazaji wa kituo kimoja cha radio ya dini anasema tangu akiwa mdogo amekuwa ni mtu anapenda mitindo na kupendeza.

Anasema alikuwa anaumia pale ambapo anapopeleka nguo kwa fundi lakini anasumbuka kuipata.Yeye alitamani sana kuwa mbunifu wa mavazi yake na kutaka kufanya biashara ya namna hiyo ili imuongezee kipato.

Changamoto kubwa ilikuwa kupata muda wa kutosha wa kufanya kazi hiyo ya kushona bila kuingilia kazi aliyoajiriwa. Lakini jambo lingine likawa ni kuwa na ujuzi wa kufanya kazi hiyo.

Anasema aliamua kuanza kujifunza katika ofisi ya kushona ya jirani na kununua cherehani ambayo alikuwa anafanyia mazoezi.

"Haikuwa kazi rahisi kujifunza kushona na hapo hapo nnaenda kazini, kwa kipindi cha mwaka mmoja nikitoka kazini saa kumi nnaingia kwenye darasa la ufundi na nilikuwa nashangaliwa na wengi inakuwaje nmemaliza chuo kikuu na nina ajira ila bado nko kwenye kibanda cha fundi najifunza kushona."

"Kwa sasa ninafurahi kwamba nimeweza kutengeneza jina la ofisi yangu binafsi na kuepuka usumbufu wa mafundi."

Wakati Bahati Mandoa ni mwanasheria kitaaluma, kwa sasa ni mjasiriamali anayeuza korosho.

Bahati anasema hakukosea wala kupoteza muda aliposoma sheria maana sheria hiyo aliyosoma darasani inamsaidia hata sasa kuongeza thamani ya bidhaa anayouza, maana biashara ya korosho zake zina utofauti mkubwa na wauza korosho wengi.

Philomena Malenda ni mshauri wa mambo ya fedha.Yeye anaamini kwamba wanawake wanapaswa kutumia muda wao wa mapumziko kwa kujiongezea kipato na kusema yeye binafsi ni mfano halisi ambapo huzitumia siku kuu kufanya ujasiliamali .

Image caption Philomena Malenda anauza pilipili za kuzindika,Darphin Manai anatengeneza unga wa lishe na Bahati Mandai anauza korosho

"Vijana wengi huwa na kasumba kwamba mtu ukimaliza shule tu na kuandika cv basi unaweza kuajiriwa jambo ambalo sio la kweli", anasema Francisca Binamungu ambaye kwa sasa anatengeneza sare za shule, hospitali na ofisi mbalimbali.

Aidha kitu ambacho kilimvutia kufanya ujasiriamali ni kutokana na tatizo kubwa la ajira nchini Tanzania.

"Kwa sasa nina kila sababu ya kumshukuru Mungu maana mimi pia ninatoa ajira kwa watu wengine na nmegundua kwamba sisi nguvu mpya tunapaswa kutumia utaalamu tuliopata shuleni kuleta maendeleo", anaongeza Francisca.

Jambo hilo la kujiajiri na kuwaajiri ambao wana uhitaji zaidi ni jambo ambalo Evelyn Muheto mwenye shahada ya pili ya biashara analifanya kwa majirani zake ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Evelyn anasema anawaalika akina mama kumi na tano mpaka ishirini kwa wiki mara moja .

"Wanawake wengi wamezaa mapema na hivyo huwa wanakuja kufanya kazi wakiwa na watoto wao na sasa nimeanzisha mradi unaoitwa 'one child a month'ambao unamsaidia mtoto mmoja kwa huduma ya bima ya afya"

Image caption Evelyn Muheto anashirikiana na wanawake wanaoishi katika mazingira magumu kufanya ujasiriamali

Meneja mafunzo ya wajasiriamali kutoka Brac Tanzania, Namala Samson anasema shirika lao linalolenga kuwawezesha watu kujikwamua kutoka kwenye umaskini na kati ya watu milioni nne wanaowasaidia kwa mafunzo na mikopo, wanawake ni zaidi ya asilimia themanini ndio wamejitokeza kushirikiana nao na wanajitahidi sana kutekeleza masharti ya kuwa wajasiriamali wazuri.

"Vilevile wanawake wamekuwa waaminifu sana katika kurejesha mikopo kwa wakati hata kama wapo kwenye vikundi wanaweza kushirikiana katika mambo ya fedha kiurahisi"anasema Namala.