Korea Kaskazini yaanza kubomoa kituo cha kurushia makombora cha Sohae

Roketi ikirushwa kutoka eneo la Sohae katika picha hii ya KCNA Pyongyang, 7 Februari 2016 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Korea Kaskazini imekuwa ikitumia kituo chake cha Sohae kurushia roketi na makombora

Korea Kaskazini inaonekana kuanza kuondoa sehemu muhimu ya mitambo yake ya ulipuaji wa makombora kaskazini magharibi mwa taifa hilo.

Picha za satelaiti zilizoonekana na makundi 38 ya uangalizi yanayoshirikiana na Marekani,zimeonyesha harakati hizo za kuondoa mitambo hiyo, hali inayoonyesha kwamba huenda Pyongyang imeanza kutekeleza ahadi ya mwezi Juni, pale kiongozi wa taifa hilo alipokutana na Rais Donald Trump.

Korea Kaskazini imekuwa ikisisitiza kwamba kituo hicho chake eneo la Sohae ni cha kutumiwa kurushia satelaiti pekee lakini watalaamu wa masuala ya silaha wanasema kimekuwa pia kikitumiwa kufanyia majaribio makombora.

Rais Donald Trump amesema kiongozi wa Korea Kaskazini aliahidi kuharibu mitambo ya majaribio ya silaha japo kuwa hakubainisha ni mitambo ipi hasa.

Katika mkutano wao viongozi hawa wawili uliofanyika Singapore Trump na Kim Jong-un walisaini makubaliano ya kushirikiana katika kuondoa silaha za nyuklia katika eneo la rasi ya Korea.

Lakini mpango huo huo ulikosolewa kwa madai kuwa hauna muda maalumu ulipangwa kwa utekelezaji.

Hapo jana Rais Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter ameelezea kufurahishwa kwake na ushirkiano na Korea Kaskazini katika utekelezaji wa mpango huo.

Mada zinazohusiana