Je ni kweli usawa wa kijinsia unawaongezea nguvu ya kimamlaka wanawake?

Wanawake Haki miliki ya picha Getty Images

Kwamba wanaume wengi wanashikilia nyadhifa za uongozi kuliko wanawake si jambo ambalo hushangaza watu wengi.

Lakini cha kushangaza na tofauti na matarajio ya wengi ni kuwa si kweli kwamba pale panapokuwepo na usawa wa kijinsia kwenye uongozi na mambo yote pia huwa sawa.

Mataifa mengi hujaribu kujitokeza katika juhudi zao za kuwapa nyadhifa kubwa kubwa za uongozi wanawake.

Kwa mfano, Rwanda ambayo iliwapa wanawake nusu ya vyeo katika baraza lake la Mawaziri. Hivi karibuni hatua kama hiyo imechukuliwa na nchi ya Ethiopia.

Kwingineko, duniani kuna mifano tele ya wanawake kuwa sawa na wanaume na hata mara nyingine kufanya kazi nzuri mno kuliko wanaume, kuwa na nguvu na hata ushawishi.

Ingia mahakamani nchini Slovenia na utawakuta majaji wa kike kuwa mara nne zaidi ya wa kiume. Katika taaluma ya habari, Namibia imebobea: nusu ya vyeo vya juu katika vyumba vya habari vinashikiliwa na wanawake.

Sio vigumu kupata mataifa mengine yanayopiga hatua kama hizi kwenye kazi na taluma fulani. Nusu ya watalamu wa mitambo yaani IT nchini Malaysia ni wanawake, sambamba na kila wataalamu 10 wa fani ya utafiti wa matibabu nchini New Zealand sita ni wanawake. Kati ya wahandisi 10 nchini Oman basi utakuta watano ni wanawake.

Wanawake wanaoshikilia nyadhifa katika kazi ambazo mara nyingi hufanywa na wanaume, wanazidi kuongezeka na kukaribishwa.

Japo yawezekana kuwa ni jambo la kupigia mfano kwa nchi nyengine kujifunza kutokana na nchi zilizopiga hatua kwenye kukwamua wanawake, lakini swali la msingi la kujiuliza ni kuwa ushawishi wa wanawake hao uko wapi?

Nguvu ya majaji

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ruth Bader Ginsburg ni mmojawapo wa majaji watatu wa kike katika mahakama ya juu zaidi nchini Marekani

Bado katika fikra za watu wengi kuna utata wa kuapishwa Jaji wa mahakama ya juu nchini Maekani Bw Brett Kavanaugh, licha ya kuwepo kwa madai ya kuwakandamiza wanawake kimapenzi, swala ambalo amelikanusha kwa kinywa kipana.

Mahakama hiyo ambayo majaji watatu kati ya tisa ni wanawake- ni mfano wa mfumo ambao majaji waandamizi, wanashikilia nguvu kubwa sana.

Nchini Uingereza, mfumo wao wa kisheria ambao hutumika katika nchi nyengine za Jumuiya ya Madola, majaji huteuliwa katika miaka ya kilele ya utumishi wao na mara nyingi kupitia mitandao iliyosheheni wanaume. Sheria za Uingereza na nchi za Jumuiya ya Madola hutegemea uamuzi na busara za majaji.

Katika mataifa mengine kama vile Ufaransa na Slovenia, nguvu za majaji zimefinywa mno. Katika mifumo yao ya sheria majaji wana nguvu ndogo ya kutumia busara zao ili kufanya tafsiri zao wenyewe za sheria na hukumu.

Wanawake wanaouawa siku moja sehemu tofauti duniani

Na njia ya kupatikana kwao ni tofauti pia. Wahitimu wa mafunzo ya sheria huwa majaji kwa kupita mitihani yenye ushindani mkubwa, ili kuingia moja kwa moja kwenye mafunzo ya ujaji mara baada ya kufuzu.

Majaji 6 kati ya 10 nchini Ufaransa ni wanawake, lakini cheo hicho huja na kushuka kwa malipo. Mara nyingi mawakili wanaofanya kazi binafsi hupata mishara minono kuliko majaji.

Asilimia kubwa ya majaji wa kike wamo katika nchi zilizokuwa majimbo ya utawala wa Kisovieti. Kwa mfano Slovenia, Romania na Latvia kati ya majaji 10, 7 ni wanawake.

Chini ya utawala wa ukomunisti, mamaji si tu kwamba walikuwa wanapata malipo duni, lakini pia walikuwa wanabanwa na misingi ya kiitikadi. Hadi sasa idara ya mahakama katika mataifa hayo ina sifa duni na majaji wangali wakipata mishahara midogo.

Baada ya mageuzi

Katika taluma nyingine, wanawake wanazidi kupata nguvu, hasa kufuatia kipindi cha mabadiliko ama mageuzi.

Kwa mfano, chini ya sera za ukomunisti nchini Bulgaria, uandishi habari ulikuwa chini ya serikali. Lakini baada ya mwaka 1989, uhuru wa habari ulikuwa kwa kasi na wanawake wengi waliokuwa wamesoma na wajasiriamali walibadilisha mikondo ya taaluma zao na kujiunga na vyumba vya habari, na idadi yao kupanda na kuwa sawa na wanaume.

Nchini Rwanda swala la usawa wa kijinsia Bungeni lilianzishwa mwaka 2003. Hatua hiyo ilitoka baada ya kuharibiwa kwa taasisi za serikali wakati wa mauaji ya kimbari yalitokea nchini humo mwaka 1994.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa Rwanda Paul Kagame na wabunge wapya 80 mwezi Septemba, 2018

Wabunge sita kati ya 10 nchini Rwanda ni wanawake, hatua inayoiweka nchi hiyo ndogo ya Afrika kuwa katika nafasi ya kwanza duniani.

Lakini huko pia, kuna maswali mengi kuhusiana na ni nani hasa anayeshikilia mamlaka kubwa zaidi ya taifa.

Mfahamu Mungu asiyetaka wanawake India

Kiongozi mkuu nchini Rwanda Bw Paul Kagame, ameshutumiwa kwa kuongoza taifa kwa mkono wa chuma. Wengi wamedai kuwa, kuwepo kwa wabunge wengi wa kike, hakutoi fursa yoyote ya kugawana mamlaka.

Lakini kwa upande mwengine kuna wale ambao wandai kuwa uwepo wa wanawake wengi bungeni una manufa makubwa kwenye jamii ikiwemo kuheshimiwa wananawake kuanzia kwenye familia na nguvu ya kushawishi maamuzi ya nchi.

Je, hii yote ina maana gani?

Uhusiano kati ya wanawake na nguvu ya kimamlaka ni mgumu kuutolea hitimisho sahihi kwa kuangalia takwimu yoyote ile - ni muhimu kuangalia suala hili kwa muktadha mpana.

Japo yawezekana kuwa safari ni ndefu lakini ni dhahiri kuwa na wanake wengi viongozi - hata kama si watimilifu - ni alama ya kukua kwa nguvu yao, na yaweza kufanya watu kukubali kuongozwa na wananwake.

Hata hivyo, jambo moja na la muhimu lipo wazi: pale mambo yanapofanywa kwa namna ambavyo yamekuwa yakifanywa kila siku, mabadiliko - iwapo yatatokea - basi huwa ya taratibu.

Mada zinazohusiana