Uharamia Somalia: Namna manowari na ndege za kivita za mataifa ya magharibi zilivyodhibiti uhalifu pwani ya Somalia

Meli ya kivita ndani ya pwani ya Somalia
Image caption Doriaza kijeshi kupitia manowari na helikopta zimeshika kasi katika pwani ya Somalia

Visa vya uharamia katika pwani ya Somalia vimepungua sana, ripoti ya hivi karibuni ya BBC inaonesha kuwa manowari za mataifa ya magharibi zimechangia pakubwa kudhibiti uhalifu huo uliotikisa dunia.

Katika ufukwe wa Hordeia uliopo katika pwani ya ya Somalia mwanahabari wa BBC Anne Soy alikutana na haramia mmoja wa zamani ambaye alieleza ni kwa namna gati alijikuta akiingia kwenye shughuli hiyo ya haramu.

Mwanamume huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, awali alikuwa mvuvi, na alitumia kazi hiyo kama kitega uchumi, lakini hali ilibadilika baada ya wavuvi haramu kuharibu nyavu zake kwa kutumia mashua kubwa za uvuvi kuvua samaki.

"Walipitia juu ya nyavu zetu, na kuzivuta. Zana zetu za uvuvi ziliharibiwa," anaeleza na kudai kuwa juhudi zake pamoja na wavuvi wenzake kudai haki hazikufua dafu. Walibaki na hasira pasi na malipo yoyote.

Hatua waliyoichukua baadae ilikuwa ni mwendelezo wa matendo ambayo si tu yaliitikisa dunia bali kufanya pwani ya Somalia moja ya njia hatari za usafiri wa bahari na kutishia biashara ya mabilioni ya dola.

Waligeukia uharamia, kuteka nyara meli na kuwazuilia mabaharia ili kulipwa pesa za kikombozi.

Si wavuvi tu, bali wanamgambo wa zamani waliokuwa wakipigana chini ya wababe kadhaa wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia pia waliingia kwenye shughuli hiyo ovu.

Image caption Wavuvi wanaombwa kurejelea biashara yao ya uvuvi

BBC ilipotaka kufahamu zaidi maisha yake alipokuwa haramia, aliingiwa na wasiwasi na ghafla akakatisha mahojiano.

Kilichoonekana kumtia wasiwasi, ni askari mmoja wa kikosi maalum cha Uhispania ambaye alikuwa akipiga doria karibu.

Usalama ndani na nje ya ufukwe ulikuwa mkali huku helikopta ikipaa angani. Ndege hiyo ni sehemu ya vikosi vya wanajeshi wa Mataifa ya Jumuia ya Ulaya maarufu kama (EUNavfor).

Image caption Kuwepo kwa meli za kivita za kigeni zimefanya pwani ya Somalia kuwa salama

Hiyo ni ishara thabiti kuhusiana na mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika miaka ya hivi karibuni, na kupunguza kwa kasi vitendo viovu vya uharamia.

Mwongo mmoja uliopita, maharamia walikuwa wakitekeleza uovu wao huko kiholela, na kulikuwa na maficho kadhaa kote pwani ya Somalia, kama vile Eyl, mji mmoja mdogo wa bandari nchini Somalia inayomilikiwa sasa na utawala wa jimbo lililojitangazia uhuru wake la Puntland.

Njia hatari ya baharini

Wakaazi wa mji huo waliiambia BBC kuwa miaka ya nyuma ambayo pesa zilijaa tele kwenye masoko ya hapo, na kufanya hali ya maisha kupanda kwa kasi.

Licha ya kuwa na silaha ambazo ziliwatisha wananchi ilikuwa ni vigumu mno maharia kumuuwa mtu.

Pia walikuwa wakiwazuilia baadhi ya mabaharia, waliowateka nyara na kisha kuitisha pesa nyingi za kikombozi, mara nyingine mamia ya dola na hata mara nyingine maelfu ya dola.

Image caption Ramani ya taifa la Somali

Kuwepo kwa utajiri mkubwa huenda ndicho kiini hasa kilichowasukuma maharamia hao katika pwani ya Somalia.

Lakini kukosekana kwa utawala nchini humo, tangu kusambaratika kwa serikali ya Rais Siad Barre mwaka 1991, na kuvunjiliwa mbali kwa jeshi la majini la Somalia, kulichangia pakubwa kuongezeka kwa uharamia.

Maji ya mipaka ya Somalia, pia ilishuhudia vitendo vya wizi mkubwa wa samaki, mashua za magendo, utupaji taka baharini na uharamia.

Njia ya meli inayopitia bahari Hindi kupitia Somalia, ikawa mojawepo ya njia hatari sana duniani.

Lakini miaka 10 baadaye, Muungano wa Bara Ulaya-EU, shirika la kujihami la mataifa ya magharibi NATO na mataifa mengine duniani, yakaamua kutuma vikosi vyao vya kijeshi hadi eneo hilo, mara baada ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha meli za kivita kwenda hadi maeneo ya maji ya mpaka wa Somalia.

Mashambulio ya maharamia yamedhibitiwa, baada ya kufukia kilele mwaka 2011.

Image caption Takwimu ya mashambulio Pwani ya Somalia

Mwandishi wa BBC alipata fursa ya kuona mabadiliko hayo kutokea mstari wa mbele kwa kuabiri kwa siku saba ndani ya meli ya kijeshi ya Uhispania kwa jina ESPS Castilla, ambayo ni sehemu ya meli za kijeshi zinazotoa ulinzi baharini chini ya muungano wa EUNavfor.

Katika siku ya pili kwenye meli hiyo, kiamsha kinywa kilikatizwa, na waandishi wetu kuelekezwa hadi kwenye daraja la meli. Boti moja ilikuwa imeonekana kwa umbali baharini.

"Hatudhanii kuna kitu chochote cha kutiliwa shaka, lakini tulizidi 'kusogea kirafiki' kama sehemu ya kupiga doria baharini," Afisa mmoja alisema.

Baada ya mkutano mdogo wa haraka haraka, wanajeshi wa majini wapatao watano hivi, mara moja wakashuka kutoka kwenye meli ya kijeshi na kuingia ndani ya maboti yaliyokuwa karibu yakisubiri.

Hifadhi kubwa ya samaki

Mara tu Manowari hiyo ya Uhispania ilipowafikia wavuvi hao, msako mkali wa haraka ukafanywa.

"Chombo hicho cha majini kinatokea Yemen lakini wengi wa mabaharia ni Wasomali," Afisa aliyeongoza msako aliezea baada ya kusikiza mawasiliano ya redio.

Wavuvi walikuwa 8 wakati huo walikuwa wametulia wakibarizi tu huku wakinywa maji ya chupa waliyopewa na wanajeshi hao maalum wa Uhispania.

"Kuna soko zuri la samaki nchini Yemen, ndio maana tunauza samaki wetu huko," Osman Ali mmoja wa wavuvi akasema.

Image caption Wavuvi wanasema usalama umeimarika tangu EU ilipotuma vikosi vyake vya kijeshi

Anasema alikuwa akivua samaki pwani ya Tanzania, lakini akavutiwa na maeneo ya Kaskazini zaidi kutokana na wingi wa samaki katika maji ya pwani ya Somalia. "Lakini sijawaona maharamia kabisa," alisema huku akijawa na uoga, na kisha akabadilika mara moja kwa kutozungumzia swala hilo.

Wavuvi wote wanaoendesha shughuli zao hapa wanafahamiana, na kukiwepo na swala la usalama mara moja wanawafahamisha wenzao na kisha wanahamia maeneo salama, aliongeza.

"Mara nyingine tunakutana na watu wabaya ambao wanaiba zana zetu za kazi, lakini kuwepo kwa meli za kivita hapa, hali inazidi kuimarika," Bw Ali alisema.

Boti ililipuliwa

Juzi tu, taarifa ilitufikia kuwa, meli moja ya mizigo ilishambuliwa maili 300 Mashariki mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Boti moja dogo, au mtumbwi, ulikaribia meli karibu mita 50 na kisha kuishambulia, lakini walinzi walioko kwenye meli walikawakabili, kwa risasi na kuwatishia kisha wakatoroka.

Ni vigumu sana kushambulia meli ya kijeshi ya Castilla, lakini siku iliyofuatiwa mtumbwi huo ulifuatiwa hadi pwani moja ambayo inaaminika kuwa na maharamia.

Wanajeshi wa Uhispania, walivuta mtumbwi huo hadi baharini na kisha wakaulipua.

Ni kisa cha pili kuripotiwa mwaka huu wa 2018. Mashambulio yote hayakufua dafu.

Katika mji wa Eyl, uhasama ulimalizwa huku maharamia wakifurushwa au kuuwawa.

Image caption Kikosi cha polisi wa jimbo la Puntland ni kidogo mno

Kurejelea Uvuvi

Kamanda mkuu wa polisi mjini Eyl, Mohammed Dahir Yusuf ana matumaini kuhusiana na uwezo wa mji huo kukabiliana na uhasama wowote wa maharamia kuchipuka tena.

"Boti yoyote ya maharamia hushikwa mara moja na askari wa majini na kuletwa hapa kwa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wale wanaokiendesha chombo hicho."

Kikosi anachokizungumzia Yusuf kina askari 800, japo ni kikosi kikubwa, lakini uwezo wake ni finyu.

"Hatuna boti za kutosha kufanya doria kali baharini," amesema bw Yusuf.

Kwa sasa, wengi wa walioukuwa maharamia wamerejea kwenye uvuvi, lakini, wachambuzi wa masuala ya usalama wa EU wanaonya kuwa bado ari ya kuendelea na uharamia pale nafasi itakapopatikana.