Uingereza : Kampeni ya kupinga matumizi ya dawa za kuongeza ukubwa wa midomo na upasuaji kuanzishwa

Madhara ya kuongeza ukubwa wa mdomo

Chanzo cha picha, RACHAEL KNAPPIER

Maelezo ya picha,

Madhara ya kuongeza ukubwa wa mdomo

Kampeni maalum ya kupinga upasuaji wa kubadili muonekano wa maumbile umeanzishwa hivi karibuni nchini Uingereza.

Kampeni hii imekuja mara baada ya ongezeko la watu wanaofanya upasuaji wa kubadili maumbile yao kusababisha vifo.

Kumekuwa na tahadhari juu ya ongezeko la watumiaji sindano za dawa ambazo zimekuwa za kuongeza muonekano wa mdomo, kwa hofu kuwa kuna madhara ambayo yanaweza kutokea.

Mtaalam mmoja amepokea kampeni hiyo na kutaka mamlaka kuchukua hatua inayohitajika ili kukemea tabia hiyo.

Vipindi maalum vya kampeni hiyo vitaanza baada ya wiki mbili ili kuhakikisha kuwa umma ina taarifa muhimu juu ya umuhimu wa kutafuta wataalamu wa afya kabla ya kufanya upasuaji au kutumia dawa ya kuongeza muonekano.

Kampeni hiyo ina matumaini ya kutokomeza matumizi kadhaa ya ubadilishaji wa maumbile ambayo yanapelekea mtu kuathirika na afya ya akili na vilevile kuepuka gharama kubwa ya matibabu.

Huku mtaalamu mwingine amesema elimu juu ya ubadilishaji huo wa maumbile bado haujaweka wazi kuhusu madhara makubwa ambayo yanaweza kuwapata wanapotumia dawa hizo au wanapofanya upasuaji usipofanikiwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Watu maarufu kama Kylie Jenner wameanza kusaidia kuhamasisha juu ya madhara ya dawa za kuongeza ukubwa wa midomo.

Watu maarufu na wenye ushawishi wameguswa na kampeni hiyo na kuanza kushiriki kutoa elimu hata kueleza kile ambacho kilichowapata walipofanya mabadiliko hayo katika miili yao.

Ikiwa namna ya kuhamasisha watu waweze kuwa na ueleo kwa urahisi zaidi.

Maumivu makali hujitokeza baada ya muda mrefu kupita

Greg ambalo si jina lake halisi ameiambia BBC kuwa alipata uraibu wa kutumia sindano za dawa hiyo ili kung'arisha ngozi yake ingawa dawa hiyo huwa inatumika ili kuongeza ukubwa wa midomo na mashavu.

Greg anasema alianza kutumia dawa hizo miaka mitatu iliyopita na sasa ameanza kupata madhara ya kutoona vizuri n ahata muonekano wa sura yake kutovutia.

Madhara yalianza kujitokeza siku moja alipoamka asubuhi na kuhisi maumivu makali sana na mdomo wake kuongezeka kuwa mkubwa zaidi.

"Maumivu yalikuwa makali sana na nilikuwa naona aibu kutafuta msaada,"Greg alisema.

Greg aliongeza kusema kuwa hawezi kumshauri mtu yeyote kutumia dawa ili kuongeza ukubwa wa midomo yake.

"Ni muhimu kujua madhara ambayo unaweza kupata na kuwa makini sana."

Bi. Nugent,ambaye ni mtaalamu wa upasuaji huo anasema watu wengi wanaofanya urembo huo huwa hawapati mafunzo ya sahihi ya afya.

Na hali hii inapelekea mtu kuanza kutumia dawa au kufanya upasuaji bila ya kujua athari ambazo zinaweza kumpata na namna ambavyo anaweza kujitunza asipate madhara au kugundua mapema athari zinapoanza kujitokeza.

Kuna mambo ambayo mtu anapaswa kuzingatia kabla hajaanza kutumia mfumo huo.

Na mtu yeyote ambaye anapenda kutumia urembo wa aina hiyo inabidi achukue muda kutafuta inayomfaa, salama na iliyoshauriwa na mtaalam wa afya na kuhakikisha kuwa wanaelewa athari ambazo zinazoweza kujitokeza..

Tangu mwaka 2017 -18,wagonjwa 934 walikutwa na matatizo yaliyosababishwa na upasuaji au utumiaji wa sindano yenye dawa kubadili muonekano na kati ya wagonjwa hao 616 walikuwa wametumia dawa ya kuongeza ukubwa wa midomo.