Uchunguzi wa BBC: Njaa yawauwa wafungwa ndani ya magereza ya DRC

Maafisa wa gereza pia wamekuwa wakiwabaka wanawake katika magereza ya DRC Haki miliki ya picha AFP

Miongoni mwa changamoto kubwa ambazo zimekuwa zikizungumziwa katika Jamuhuri ya kidemokrasi ya Kongo umekuwa Ebola na mapigano ya mashariki mwa nchi.

Lakini kuna changamoto kubwa ambayo imesahaulika na kupuuzwa nayo ni ripoti zinazotolewa juu ya vifo vya wafungwa wanaokufa ndani ya magereza mbali mbali nchini humo kwa kiwango kikubwa. Katika mji wa Mbanza Ngungu takriban wafungwa 40 walizikwa mwezi machi pekee, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC wa mjini Kinshasa Emery Makumeno aliyefanya uchunguzi kwenye gereza hilo.

Jela la Mbanza Ngungu linaonekana kama lundo la matofali mekundu yaliyozeeka.

Wafungwa katika jela hilo husimama wakati wote kwenye nyuma ya vizuwizi vya vyuma wakiwa vifua wazi, anasema Makumeno. BBC haikuruhusiwa kuingia ndani wala kuchukua viedeo wala sauti yoyote ilipozuru gereza la Mbanzangungu.

Wanajeshi makumi kadhaa wenye silaha nzito nzito hulinda gereza usiku na mchana.

Joceline Bikendu, mwenye umri wa miaka 23, ambaye alifungwa mwaka mmoja kwa mashtaka ya ukatili anasema alipokuwa katika gerezani alikuwa mjamzito na anasema alikwa akilazimika kuwaomba wapita njia kitu cha kula kupitia shimo dogo lililokuwa kwenye ukuta wa gereza la Mbanza Ngungu.

"Ningeweza kukaa siku nzima bila chakula. Nilikuwa nasikia mtoto akicheza tumboni nahisi kuzunguzungukabla ya kulala. Gereza lilikuwa linatupatia kiwango kidogo sana cha unga wa muhogo kupika ugali lakini hata mtoto mchanga asingeweza kushiba".

Wahudumu wa gereza walituambia kuwa wafungwa hupata mlo mmoja kwa siku wa ugali wa muhogo kwa majani ya mihogo (kisamvu). hakuna nyama wala samaki, na senti 20 tu hutumiwa kwa gharama ya chakula cha mfungwa mmoja. Lakini kiasi hicho ni robo tu ya gharama za mfungwa kulingana na sheria.

Mara nyingi Joceline anasema wanapokosa chakula kwa mwezi mzima , ndipo wafungwa wengi hufa.

Hakuna ugali wa muhogo, hakuna kisambu, tulikuwa tunalazimika kujilisha wenyewe. Katika kitengo cha wanaume watu walikuwa wanakufa . Watano au sita kila siku . Walikuwa wanashindwa hata kutembea kutokana na njaa. ulikuwa unawasikia wakilia mchanana baadhi ya wafungwa wenzao walikuwa wanasaidia kuwalisha kidogo walichopata"

BBC ilishuhudia makaburi yaliyokuwa na misaraba 45 iliyoonekana ikiwa mipya, lakini hayakuwa na maua. Majina ya marehemu yaliandikwa na kalamu yenye wino mweusi.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Baadhi ya Magereza nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yanaripotiwa kujaa kupita kiasi wafungwa wa kisiasa ambao mara kwa mara wamekuwa wakiteketeza moto magereza na kutoroka

Marehemu wote walikuwa wamezikwa katika kipindi cha siku mbili mnamo mwezi machi mwaka huu.

Waraka uliokuwa kwenye hifadhi ya maiti ulioshuhudiwa na BBC - unaonyesha kuwa wafungwa wote 45 walikufa katika kipindi cha siku katika kipindi cha miezi 18 kati ya mwaka Septemba 2017 na Machi 2019.

Didier Nsimba,Naibu mkuu wa wilaya ya Mbanza-Ngungu, anasema mazishi ya pamoja ya wafungwa yaliandaliwa kutokana na mipango ya uchaguzi wilayani humo.

"Mkoa ulikuwa na mambo mengi ya kufanya, mazishi ya wafungwa hayakuwa kipaumbele ''.Alisema Nsimba.

Ni vigumu kubaini hasa ni nini sababu ya kifo kwa kila mfungwa kwasababu daktari alikataa kujibu maswali ya BBC. Lakini duru za mahakama ziliiambia BBC kwamba wafungwa hao hawakuweza kutembelewa na familia zao ambazo zingewaletea chakula.

Aliposhinikizwa kwa maswali, Didier Nsimba alikiri kuwa utapiamlona hali mbaya kwa ujumla kwenye magereza ndio sababu za vifo vya wafungwa, lakini akasema kuwa gereza linakabiliwa na changamoto kubwa za kifedha.

"Magereza yametelekezwa . Magereza yapo, watawala wa magereza wapo, lakini ni zipi raslimali walizopewa? Hatuna raslimali. Wafungwa hawa hawakuwa na chakula cha kutosha, na wengi walikuwa hata hivyo wanaumwa. Unakuta baadhi wamekufa kwa malaria, homa ya matumbo nakadhalika ."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Baadhi ya maafisa wa kijeshi pia walipatikana na hatia ya kuwabaka wanawake wafungwa

Mkurugenzi wa gereza hakutaka kurekodiwa wakati wa mazungumzo na BBC. Lakini alisema kuwa wafungwa walikula mara moja kwa siku, hawakufa kutokana na ukosefu wa chakula , bali walikufa hasa kwa magonjwa .Na akasema kituo cha afya kilichopo karibu kilikosa vifaa na wahudumu wa afya wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya kiafya ya wafungwa.

Kwa mwanaharakati wa haki za binadamu Victor Nzunzi, ambaye hutembelea gereza la Mbanza Ngungu mara kwa mara, maafisa wa serikali hawasaidii vya kutosha wanaopoitwa kusaidia kwenye gereza. Anasema hali katika gereza hilo ni mbaya sana: ''Gereza linapaswa kuwa na wafungwa 150,lakini idadi iliyomo ni mara dufu ya hiyo'', alisema.

Hali katika gereza la Mbanza Ngungu si tofauti sana na magereza mengi katika jamuhuri ya Kidemokrasia ya kongo. Mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakilalamikia hali mbaya, lakini bado wafungwa wanaendelea kuteseka. Mateso ndani ya jela yamekuwa yakiwafanya wafungwa wengi kutoroka magereza hususani katika maeneo ya mashariki mwa taifa hilo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii