Tanzania: IGP Sirro asema jeshi lake lilipata fununu za tishio la ugaidi kabla Ubalozi wa Marekani

IGP Simon Sirro
Image caption IGP Simon Sirro

Mamlaka za usalama nchini Tanzania zimewatoa hofu wananchi juu ya tishio la ugaidi katika maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam, zikisema zilikuwa na taarifa hizo na kwamba zimeshaanza kufanyiwa kazi.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) nchini Tanzania, Simon Sirro amesema kuwa jeshi lake lilishapata fununu za shambulio hilo kabla Ubalozi wa Marekani kutoa tahadhari juu ya tukio hilo kupitia tovuti yake Juni 19,2019.

Kuhusu tahadhari iliyotolewa na ubalozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Sirro alisema: "hiyo ni taarifa kama taarifa nyingine, inaweza kuwa ya kweli au uongo, lakini sisi kama vyombo vya ulinzi huwa hatupuuzi jambo''.

Aliongezea kuwa walipata taarifa kuhusiana na tishio hilo Tangu siku ya Jumanne Juni 17, 2019 tulipata na kwamba timu zao za operesheni na intelijensia na wengine wanaifanyia kazi.

Katika tangazo lake Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tahadhari kuwa kuna fununu za mipango ya mashambulizi jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa tahadhari hiyo iliyochapishwa kwenye kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya Ubalozi huo, eneo la Masaki ndilo linalolengwa.

Eneo hilo lililopo kwenye rasi ya Msasani ni moja ya maeneo ya makazi ya kigahari zaidi jijini humo.

Tahadhari hiyo inabainisha kuwa, maeneo yanayolengwa ni mahoteli na migahawa ambayo hutembelewa na watalii ikiwemo eneo maarufu la maduka ya Slipway.

"Ubalozi hauna ushahidi wa moja kwa moja wa tishio hilo ama taarifa za muda gani mashambulizi yatatokea, hata hivyo unawaonya wananchi kuchukua tahadhari."

Ubalozi huo aidha umewataka wakazi, kujiepusha na makundi na kufuatilia taarifa kupitia vyombo vya habari.

Huwezi kusikiliza tena
Angalizo la shambulizi la kigaidi Tanzania lina maana gani?

Kumbukumbu ya Mashambulizi ya mwaka 1998

Miaka zaidi ya 20 iliopita wapiganaji wa jihadi walishambulia kwa pamoja balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania, na kuanzia wakati huo Ugaidi umeendelea kukita mizizi Mashariki mwa Afrika.

Ilikuwa tarehe 7 mwezi Agosti mwaka 1998, saa nne na nusu asubuhi, wakati wauaji wawili walilipua lori moja lililokuwa limejaa mabomu mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Nairobi, nchini Kenya.

Dakika tisa baadae bomu lengine likalipuka katika balozi nyengine ya Marekani mjini Dar es Salaam katika nchi jirani ya Tanzania.

Takriban watu 242 waliuawa katika mashambulizi hayo mawili yalioharibu kabisa balozi hizo za Marekani na kusababisha kuporomoka kwa nyumba zilizokuwa karibu.

Matukio hayo ya mashambulizi hayakutarajiwa, sio tu kwa Wakenya na Watanzania lakini kwa dunia nzima.

Hakujawahi kushuhudiwa waathiriwa wengi namna hiyo katika shambulio lililofanywa na mtandao wa magaidi wa Al Qaidi ambao hata ulikuwa haujulikani wakati huo.

Awali mashambulizi ya wanamgambo wa kiislamu yalikuwa sana yakifanyika katika vituo vya kijeshi.

Lakini ghafla Osama Bin Laden na kundi lake wakajipatia umaarufu mkubwa kimataifa kutokana na matukio yao maovu.

Badhi ya wataalamu wanasema mashambulizi yao yalianzisha mwanzo wa vita dhidi ya ugaidi, kufuatia Marekani kujibu mashambulizi hayo kwa kurusha makombora dhidi ya walengwa katika mataifa mbali mbali.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii