Tuzo ya uandishi wa habari ina maana gani kwa Maxence Melo ?

Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa Jamii Forums Maxence Melo Mubyazi anasema tuzo ya CPJ) itamsaidia katika ufanisi wa kazi Haki miliki ya picha Jamii Forum
Image caption Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa Jamii Forums Maxence Melo Mubyazi anasema tuzo ya CPJ) itamsaidia katika ufanisi wa kazi

Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa Jamii Forums Maxence Melo Mubyazi, anasema kuwa tuzo ya Kimataifa ya uhuru wa habari, inamuongezea hamasa zaidi ya kuifanya kazi yake anaoyoipenda.

Akizungumza na BBC mshindi huyo wa tuzo ya kimataifa ya uhuru wa habari mwaka 2019, amesema: ''Kwa kweli kwanza itaniongezea ufanisi wa kazi ...Utendaji wangu kwa kweli Utaboreka, unajua baada ya kufanyakazi kwa juhudi zote, nimetuzwa hili linanitia moyo sana'', amesema Bwana Melo.

Tuzo hiyo ya Kamati Maalum ya Kuwatetea waandishi wa habari duniani (CPJ) hutolewa kwa waandishi wa habari waliopitia vikwazo vya kisheria.

Amesema ameshinda tuzo hiyo huku akikabiliwa na kesi mbili mahakamani ambazo baadhi ya masharti ya dhamana ni kutotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Kamati maalum ya kuwatetea waandishi wa habari duniani (CPJ) imesema kuwa Melo ambaye ni mmiliki wa na muasisi mwenza wa wavuti wa habari wa Jamii Forums, ambao ni maarufu katika nchi za Afrika Mashariki na kati, ambao hutumika kama jukwaa la mjadala na hutumika kama chanzo cha taarifa mpya na umekuwa ukitumika kutoa taarifa za siri ambazo zimesaidia kuboresha uwajibikaji na uwazi nchini Tanzania.

" Hili ni jambo kubwa kwangu nimekumbana na changamoto nyingi hasa kuhudhuria kesi mahakamani zaidi ya mara 100," amesema Melo.

Wavuti wa Jamii Forum hutumika kuendesha mijadala, hasa kwa lugha ya kiswahili, juu ya mada zikiwemo kuhusu rushwa katika sekta ya umma na mapungufu ya serikali.

Melo ambaye ameshinda tuzo hiyo huku akikabiliwa na kesi mbili mahakamani ambazo baadhi ya masharti ya dhamana ni kutotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam ameiambia BBC kuwa amefurahiwatuzo yake. '' Ninafurahi kwamba kwamba nimeweza kupata tuzo hii kwa kuitumikia jamii na kutambuliwa kwa kazi ngumu ninayoifanya kwa ajili jamii''.

Huwezi kusikiliza tena
Mwanzilishi wa Jamii Forums azuiliwa Tanzania

Mkurugenzi huyo wa Jamii Forum amekiri kuwa kazi yake sio rahisi, hata hivyo amewaomba waandishi wa habari wenzake hususan nchini Tanzania kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari badala ya kuharibiana majina.

'' Ningependa kuwaomba waandishi wenzangu tuepuke kukandamizana, kuchafuliana majina kwenye mitandao ya kijamii, halafu kama kuna taarifa tuifanyie uchunguzi kabla ya kuitangaza. Tuifanye kazi yetu kwa kujiaminisha. Bila upendeleo, tusiangalie sura, na tufahamu kuwa kazi yetu ina mipaka'', amesisitiza Bwana Melo.

Melo ametunukiwa tuzo hiyo kwa kuongoza uhuru wa kujieleza mtandaoni.

Mnamo mwaka 2016, ofisi ya Jamii Forum ilivamiwa na vikosi vya usalama ambavyo vilimkamata kwa ajili ya kuhojiwa.

Baada ya kushikiliwa kwa siku nane, Melo alishtakiwa kwa kumiliki mtandao ambao haukusajiliwa nchini Tanzania na kukataa kufichua utambulisho wa watumiaji wa Jamii Forum.

Mashtaka dhidi ya Melo yako chini ya sheria ya Tanzania ya 2015 ya uhalifu wa mitandaoni.

Mnamo mwaka 2017, Melo alifikishwa mahakamani mara 81. Hadi leo anaendelea na kesi ya kutaka kulisafisha jina lake.

Melo ni Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo hiyo tangu zilipoanzishwa mwaka 1996 na atakabidhiwa Novemba, 2019 mjini New York, Marekani.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii