Tanzania: Zoezi la kuwaondoa wakimbizi wa Burundi laanza kwa kufunga masoko

burundi Haki miliki ya picha STEPHANIE AGLIETTI

Zoezi la kuwarejesha Burundi wakimbizi wa nchi hiyo walioko kwenye kambi za wakimbizi nchini Tanzania linaendelea, licha ya kukukutana na ukinzani mkubwa kutoka kwa baadhi ya wakimbizi wasiotaka kurejeshwa.

Maduka na biashara zingine zimeanza kufungwa katika kambi hizo magharibi mwa Tanzania, kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la serikali ya Tanzania ya kuwarejesha wakimbizi hao ifikapo Oktoba mosi mwaka huu.

Zaidi ya wakimbizi 200,000 wa Burundi wanaishi nchini Tanzania, wengi wao wakitoroka ghasia nchini mwao zilizozuka mwaka 2015.

Esbomana Emanuel, ni mkimbizi kutoka Burundi anaelezea hali ilivyo sasa,

"Wameanza kufunga masoko, na ukikamtwa sokoni unakamatwa na hofu bado iko kwenye shule.

Kwa mfano mimi siwezi kusema kuwa nitaenda kwa sababu kama nitaenda labda mpaka niliwe maana niliyemkimbia suluhisho bado.

Wale ambao wako kwenye kambi za Burundi hawajarudi sasa mimi siwezi kuamini kuwa Burundi kuna amani" Emanuel anaeleza.

Lakini kwa upande wake waziri wa mambo ya ndani, Kangi Lugola ameiambaia BBC Kwamba zoezi hilo la kuwarejesha wakimbizi hao lipo pale pale, na linaendelea vizuri.

Kambi ya Nyarugusu ina idadi ya wakimbizi zaidi ya 50,000 kutoka Burundi.

Mvutano kati ya shirika hilo la wakimbizi la Umoja wa mataifa na serikali ya Tanzania kuhusu suala la kuwaregesha makwao wakimbizi wa Burundi umekuwa ukiendelea kwa miaka kadhaa sasa.

Mwezi Agosti mwaka mwaka 2017, Serikali ya Tanzania ililipatia shirika la UNHCR siku saba kuanza kuwarudisha wakimbizi wa Burundi ambao wanataka kurudi kwao kwa hiari, ama sivyo serikali ifanye zoezi hilo yenyewe.

Serikali ya Tanzania imesifiwa kwa kuendelea kubeba mzigo huu mkubwa wa wakimbizi lakini zaidi kwa kukubali kutekeleza mkakati wa kimataifa ujulikanao kama Comprehensive Refugee Response.

Ni mkakati uliolenga kutafuta namna endelevu ya kuwasaidia wakimbizi kupata ulinzi na mahitaji mengine ya msingi ya kibinadamu.

Lakini zaidi katika kutafuta namna ya kuwashirikisha wakimbizi hawa katika shughuli mbali mbali za maendeleo katika nchi wanazokimbilia.

Tanzania ndio nchi inayohifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka Burundi kuliko nchi nyingine yoyote ile katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Wakati Tanzania ikiwarejesha wakimbizi wa Burundi nchini mwao huko Uganda, idadi ya wakimbizi wa Burundi inaonekana ukuongezeka nchini humo kwa mjibu wa takwimu za Shirika la umoja wa mataifa la maswala ya wakimbizi duniani UNHCR .

UNHCR inasema kuwa mwezi wa Julai tarehe mosi hadi tarehe 31 , idadi ya wakimbizi wanaoingi nchini Uganda ilipugua kwa asilimia 32 ukilinganisha na miezi miliyopita.

Hata hivyo idadi ya wakimbizi kutoka Burundi sasa imeongeza mwezi huo kwa aslimia 121.

Takwimu kamili za wakimbizi wapya mwezi Jully waliongia nchini Uganda ni 8,295. Wakimbizi wapya waliongia kutoka DRC ni 6, 490, kutoka Sudan kusini 944 na kutoka nchini Burundi ni 861.

UNHCR inaonyesha kwamba idadi ya wakimbizi kutoka Sudani kusini na DRC imepungua na ongezeko kutoka Burundi, msemaji wa UNHCR nchini Uganda Bi Duniya Aslam Khan amethibitisha kuongezeka kwa wakimbizi wa Burundi alipozungumuza na BBC lakini amekanusha kuhusisha ongezeko hilo na serikali ya Tanzania kuwarudisha Warundi kwao.

Haki miliki ya picha AFP

Mmoja wa wakimbizi kutoka nchini Burundi ambaye yuko mjini Kampala amesema kwamba kumetokea kundi moja la siasa nchini kwao ambalo limeleta vurugu na kusababisha idadi ya warundi wengi kukimbia makazi yao lakini amekataa kutaja kundi hilo la siasa kwa sababaiu zake za ki usalama.

Ripoti hii inakuja siku chache serikali ya Uganda imetangaza kutafakari upya sera ya wakimbizi kuingia nchini Uganda, sasa hawatakubali kila mkimbizi kupata hifadhi ya ukimbizi bila kuchunguzwa , hii ni baada ya kuguduwa kuna watu wanaingia nchini kama wakimbizi huku ni majasusi.

Mpaka sasa bado Sudan kusini ndiyo ina idadi kubwa ya wakimbizi nchini Uganda ambao ni 838,323 aslimia 63.8%, DRC 365,883 aslimia 28.8% Burundi 42,334 asilimia 3.2% Wasomali 32,535 ambayo ni aslimia 2.5%. Ikiwa idadi yote ya wakimbizi kwa sasa nchini ni milioni moja na laki tatu.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii