Baadhi ya waathiriwa wa ajali ya lori Morogoro wasubiri kuwatambua wapendwa wao

Wengi wa waliopoteza wapendwa wao katika ajali ya Morogoro bado wanasubiri kuwatambua kupitia vi[imo vya vinasaba(DNA)
Image caption Wengi wa waliopoteza wapendwa wao katika ajali ya Morogoro bado wanasubiri kuwatambua kupitia vi[imo vya vinasaba(DNA)

Tanzania leo inaadhimisha mwezi mmoja tangu kutokea kwa ajali ya moto uliosababishwa na mlipuko wa lori la mafuta mkoani Morogoro ambapo watu 104 walithibitishwa kuuawa.

Baadhi ya watu waliouawa na kujeruhiwa walikuwa ni wale waliokuwa wakitaka kuchota mafuta yaliyokuwa kwenye lori lililopinduka pembezoni mwa barabara kuu ya Morogoro na Dar es Salaam na hatimae kulipuka.

Baadhi ya majeruhi ambao bado wanaendelea na matibabu na inaarifiwa wanaendelea kupona ingawa hawajaruhusiwa.

Alipotembelea eneo la tukio la mkasa huo Morogoro mwandishi wa BBC Aboubakar Famau kutathmini athari za ajali hiyo kwa wakazi wa Morogoro, alibaini kuwa baadhi ya wapita njia bado wanasimama kwa shauku na kuangalia miti iliyoungua pamoja na mchanga uliobadilika rangi kutokana na athari za moto huo.

Image caption Baadhi ya wapita njia bado wanasimama kwa shauku na kuangalia miti iliyoungua pamoja na mchanga uliobadilika rangi kutokana na athari za moto uliosababisha maafa

Wengi waliopoteza maisha yao walikuwa ni vijana waendesha pikipiki maarufu bodaboda. Familia zao, sio tu kwamba zimepoteza ndugu au waume, bali zimepoteza watafutaji wakuu wa familia.

Rehema Ramadhani alimpoteza mumewe Denis Leonard Mhima:

''Tuliendelea kusubiri arudi, lakini hakurudi, hadi tulivyofahamishwa rasmi kuhusu kifo chake majira ya saa kumi jioni. Kama unavyoona , ninaishi katka nyumba ya kupanga, ninahitaji kulipa kodi, umeme na maji, na alikuwa ndiye tegemeo la familia'', alisema Rehema huku akilia na kuongeza kuwa: ''Lakini ninawashukuru majirani zangu , wao ndio wanaonisaidia. Wakati mwingine kama mtoto wangu anapougua inanibidi nitafute njia ya kumpeleka hospitalini mwenyewe''.

Kutokana na mlipuko mkubwa wa moto uliotokea, serikali ilibidi ichukue vinasaba vya DNA kwa ajili ya kuitambua miili iliyokuwa imeharibika kiasi cha kutotambulika.

Hata hivyo, baadhi ya familia zinaonekana kuchukizwa baada ya kuona majibu ya vinasaba yanachukua muda mrefu kutoka. Ali Abdallah amempoteza mdogo yake:

''Nimempoteza ambaye mwili wake uliteketea kabisa. Tumefuatiilia matokeo ya Vinasaba(DNA) , lakini wametuahidi kuwa watatupigia simu, hadi sasa, hatujapokea simu yoyote kutoka kwao. Tuliambiwa matokeo yatatoka katika kipindi cha wiki mbili , lakini ni zaidi ya mwezi sasa. Sijui la kufanya."

Kwa upande wake, serikali inasema, mchakato mara nyengine unaweza kwenda polepole, ila inajitahidi kuwajulisha ndugu pindi majibu yanapokuwa tayari.

''Sampuli zilichukuliwa kutoka kwenye miili na ndugu wa waathiriwa kwa ajili ya vipimo vya DNA, pale tunapopata matokeo kutoka Dar es Salaam, tnawaita ndugu kwa ajili ya utambuzi wa miili. Baadhi ya matokeo bado hayajatoka bado, na pale tutakapopata matokeo tutawafahamisha''. Amesema Dkt. Rita Liyamuya Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.

Wizara ya afya ilitangaza itatoa ushauri nasaha kwa lengo la kusaidia waathirika wa ajali lakini pia ndugu wa waathirika kukabiliana na msongo wa mawazo baada ya ajali, lakini inaonekana msaada huo pia sio wote walioupata.

Abraham Mbowe ambaye anafanya kazi karibu na eneo la tukio la mkasa , anasema anasumbuliwa sana na marue rue ya mkasa huo: ''Hata leo , nilikuwa nawaambia watu kwamba sikupata usingizi . Bado naona picha za watu waliokufa zikinijia akilini, hii gereji ingekuwa inaweza kuhamishwa ningeihamishia sehemu nyingine , lakini hii ndio ofisi yangu"

Waziri Mkuu wa Tanzania Kaasim Majaaliwa ameunda tume maalumu ya kuchunguza ajali hiyo. Lakini mpaka sasa hatuna taarifa yoyote iliyotolewa hadharani kuhusiana na tume hiyo.

Hii ni miongoni mwa ajali mbaya zaidi za moto kuwahi kutokea katika historia ya Tanzania.

Kwa sasa, majeruhi, familia zao, na walioshuhudia wana safari ndefu ya kujiuguza mpaka kupona.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii