Raia wa Marekani kushitakiwa Uganda kwa kuasili mtoto kilaghai

MWANAMKE Haki miliki ya picha Getty Images

Mwanamke mmoja nchini Uganda amewapeleka mahakamani wapenzi waliochukua mtoto wake na kwenda naye nchini Marekani miaka saba iliyopita kwa madai ya kumuasili kinyume na sheria.

Mwanamke huyo mwenye mtoto wa umri wa miaka 11, anasema kuwa hajamuona wala kuwasiliana na mtoto wake tangu alipochukuliwa.

Madai ya kupinga uasili wa walezi wa mtoto huyo unakuja baada ya Robin Longoria kutoka Texas Marekani kukiri kufanya kazi na wanasheria nchini Uganda kwa kuwahonga majaji ili wageni waweze kuasili watoto.

Mwanamke huyo mwenye miaka 40 ambaye jina lake limehifadhiwa lakini tunampa jina la Jackie katika taarifa hii.

Jackie aliiambia BBC kuwa mwanae alichukuliwa akiwa na miaka mitano mnamo mwaka 2013 alipopelekwa Marekani na wazazi wake walezi, baada ya baba yake mzazi kuwakabithi raia hao wa Marekani jukumu na mamlaka ya kumlea mtoto huyo.

Inadaiwa kuwa baba wa mtoto huyo aligushi cheti cha kifo cha Jackie ili kuhakikishia mahakama kuwa mtoto huyo alikuwa akilelewa na baba peke yake katika mazingira magumu sana.

Ingawa Jackie anadai kuwa raia hao wa Marekani, mmewe na hata wakili wao wote walifahamu kuwa yupo hai.

" Ninapoishi sasa hivi ndio hapo ninaishi miaka yote, nilikuwa naishi na mtoto huyo , nilipata mimba nikiwa hapa, nilimlea mtoto wangu hapa na hata shule aliyokuwa akisoma wote wananifahamu, inakuwaje wanadai kuwa nilikufa," alisema mama huyo.

Hati za mahakama ambazo BBC imeziona, zinaonyesha kuwa Mahakama Kuu ya familia nchini Uganda ilikubali raia hao wa Marekani ambao walikuwa mme na mke kumchukua mtoto huyo ili wamlee nchini mwao.

Kwa muda huo, uamuzi wa mahakama ulikuwa unamaanisha kuwa, hata kama wazazi hawa walezi wangeishi na mtoto huyo, wazazi wake wangekubaliwa kumuona na kuzungumza naye kila mara.

Lakini, Jackie anasema kuwa amejaribu kuwatafuta kwenye mitandao ya kijamii na kupiga simu azungumze na mwanawe lakini wazazi hao walezi hawamruhusu au hata kumjulisha hali ya mtoto kama yuko salama au la.

Haki miliki ya picha Getty Images

Aidha Jackie sasa ameamua kukimbilia mahakama hiyo ya familia ili aiombe itoe uamuzi wa kurejeshwa kwa mtoto wake nchini Uganda na uasili wake kufutwa.

Denis Enap ambaye ni wakili wake Jackie anasema, wanao ushahidi utakao ihakikishia mahakama kuwa mtoto huyo aliasiliwa baada ya mahakama kutofuata sheria za Uganda.

Hii si mara ya kwanza kwa mama wa mtoto kukimbilia mahakamani ili kuomba mahakama ibadiliishe uamuzi wa kuwapa raia wa kigeni uasili wa watoto.

Mwaka uliopita, mama mwingine alishinda kesi ya kuomba binti wake arudishwe nchini na uasili wake ufutiliwe mbali.

Hali sasa imekuwa mbaya zaidi kutokana na mwanamke marekani Robin Longoria ambaye mwezi uliopita kukiri kuwahonga waamuzi wa mahakama nchini Uganda ili kuwezesha raia wa kigeni kuasili watoto kutoka uganda.

Longoria alikuwa anafanya kazi na shirika la uasili kwenye Jimbo la Ohio, nchini Marekani.

Shirika hili lilikuwa linasaidia watu kutoka Marekani kuweza kuasili watoto kutoka Uganda.

Hadi sasa, serikali haijasema itakachofanya kuhusu afisa huyo wa mahakama.

Kati ya mwaka 2014 na 2016, raia wa kigeni zaidi ya 600 waliomba kuasili watoto kutoka Uganda na 500 kati yao wallifaulu.

Mnamo mwaka 2016, sheria ya kuasili ilifanyiwa marekebisho na masharti zaidi kuongezwa ili kuwalinda watoto wanaoasiliwa hasa na raia wa kigeni.

Na tangu sheria hiyo kubadilishwa, mahakama imesikia maombi 470 na kukubali 180.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii