Tundu Lissu asitisha mpango wake wa kurudi Tanzania kwa sababu za kiusalama

lissu

Aliyekuwa Mbunge maarufu wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, ambaye alinusurika kuuawa miaka miwili iliyopita na kwenda ng'ambo kwa matibabu, amesema amesitisha mpango wake wa kurudi nchini kwa sababu za kiusalama.

Lissu, aliyetarajiwa kurejea nyumbani mwezi huu, kwenye mahojiano na kituo cha habari cha VOA Swahili huko Washington, amedai kuna matamshi ambayo yamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kumtishia.

Akizungumza kwa njia ya simu na kupitia runinga ya Chadema mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe katika makao makuu ya Chadema Lisu amesema kuwa atarudi nchini Tanzania siku hiyo ili kuadhimisha kushambuliwa kwake.

''Nitatua tarehe saba mwezi septemba 2019 kwenye ardhi ya tanzania kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa nitakuwepo, alisema Tundu Lissu

Tangazo hilo liliwafurahisha sana wanachama wa chama hicho waliokuwa katika makao makuu ya chama hicho.

Alitoa kauli hiyo katika andiko lake lenye kichwa cha habari kisemacho "Miaka Miwili ya Mateso, Matumaini".

"Nimeshakamilisha tiba kwa hiyo sababu ya kiafya ya kuendelea kukaa Ubelgiji haipo tena".

Septemba 7, 2017, Bwana Lissu alishambuliwa kwa silaha na watu wasiojulikana nje ya makazi yake Dodoma.

Maamuzi yake yamepokelewa na mtazamo tofauti na baadhi ya wananchi nchini Tanzania.

Wengi wakimlaumu kwa kuzungumza sana katika vyombo vya habari vya nje na kudaiwa kuwa anaonyesha taswira tofauti ya taifa lake.

"Hizo sababu zake hazina msingi ni kama anataka kuonyesha kuwa nchi yetu haina usalama jambo ambalo sio la kweli, huyu mtu wa kimataifa na dunia nzima inaona. Naona hicho anachoendelea kukifanya sio sawa na si kweli", mkazi wa Dodoma.

"Nahisi hizo kauli anazotoa nje ya nchi hazileti taswira nzuri kwa nchi yake, aje aongelee hayo matatizo yake nyumbani", mwananchi mwingine.

Huku wengine wakihusisha maamuzi yake na kufutwa kwake ubunge katika jimbo lake.

"Hiyo kauli haina maana sana au anasema hivyo kwa sababu kakosa ubunge, mimi naona arudi tu na kama amepata kazi nyingine aendelee nayo huko. Maana asingefutwa ubunge si angekuja tu kwa sababu ile mbinu ya kujilinda wakati akiwa mbunge anaweza kutumia pia," asisitiza mzee mmoja mkazi wa Dodoma.

Vilevile wapo wanaomuunga mkono kwa sababu waliomvamia bado hawajapatikana na haki kutendeka.

"Nadhani kwamba sababu za usalama anazozitaja ni kweli kwa sababu wale waliompiga risasi hawajakamatwa hivyo yeye kama raia ana haki ya kuamua chochote anachotaka."

Lisu adai shambulio lake lilikuwa la kisiasa

Toka wakati huo, Lissu na viongozi wengine wa upinzani wamekuwa wakilihusisha shambulio hilo na kazi yake ya siasa.

Wakati wa shambulio, Lissu hakuwa tu mnadhimu wa kambi rasmi bungeni Tanzania bali pia raisi wa chama cha wanasheria nchini humo.

Kwa kutumia kofia zake zote mbili, mwanasiasa huyo machachari alikuwa mwiba mkali wa ukusoaji wa serikali ya Magufuli.

Lissu alikuwa miongoni mwa wanansiasa wa upinzani waliopendelea kumuita Magufuli kuwa 'Dikteta Uchwara' ama kwa lugha ya kingereza'Petty Dictator'.

Baada ya shambulio hilo, alikimbizwa Nairobi kwa matibabu kisha Brussels Ubelgiji toka mwezi Januari mwaka 2018. Huko kote aliendelea kusisitiza kuwa serikali ya Magufuli ilikuwa na mkono kwenye shambulio dhidi yake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii