Mchekeshaji Idris Sultan amejisalimisha polisi baada ya kuamriwa kufanya hivyo

Idris Sultan ni mchekeshaji mwenye umaarufu mkubwa Afrika mashariki

Chanzo cha picha, Idris Sultan-Instagram

Msanii maarufu nchini Tanzania anashikiliwa na polisi jijini Dar es salaam baada ya kuweka picha yake katika mtandao wa kijamii huku picha hiyo ikiwa na sura ya rais Magufuli.

Idris Sultan alijisalimisha kituo kikuu cha polisi jijini Dar es salaam kisha kuhojiwa.

Kwa mujibu wa wakili wake Eliya Rioba, Idris amewajibishwa kwa kutumia sheria ya makosa ya mtandao kifungu cha 15 na 16 ambavyo vinaeleza kuhusu kutengeneza taswira ya kuigiza kwa kutumia kompyuta pamoja na kusambaza taarifa zenye uongo ndani yake.

Msanii maarufu nchini Tanzania aliamriwa ajisalimishe polisi baada ya kuweka picha yake katika mtandao wa kijamii huku picha hiyo ikiwa na sura ya rais Magufuli.

Mchekeshaji huyo ambaye aliwahi kuwa mshindi wa kipindi cha televisheni cha uhalisia cha 'Big Brother Africa' Idris Sultan.

Picha hizo mbili zinaonyesha kichwa cha Magufuli katika kiwiliwili huku picha moja akiwa amevaa suti huku amekaa kwenye kiti cha rais na nyingine akiwa amesimama huku amevaa mtindo wa 'suspender'.

Huku picha hizo zikiwa zinasindikizwa na ujumbe kuwa "Kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy birthday yake kwa amani".

Siku ya Jumanne,rais Magufuli alikuwa anasheherekea miaka 60 ya kuzaliwa, sherehe ambayo wananchi wa taifa hilo walitumia mitandao ya kijamii kwa wingi kutuma salamu zao kwa rais.

Unaweza pia kusoma;

Siku hiyo rais alipewa hata majina mapya labda hakuwahi kuyasikia kabla, wengine walimuita 'Mzee baba' wengine 'Jembe' na kusheheni sifa kadhaa katika vituo vya radio na televisheni.

Lakini utani dhidi ya rais uliingia ukakasi pale ambapo mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, alipotoa amri kuwa Sultan anapaswa akamatwe na polisi.

Makonda alichangia katika mtandao wa kijamii na kumtaka mchekeshaji huyo kwenda polisi.

"Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako," Makonda alisema.

Wakati huohuo waziri wa Maliasili na Utalii nchini humo Dkt. Hamisi Kigwangalla aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii akisema kuwa, "nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi."

Aliongeza kwa kuandika kwenye kurasa yake ya twitter kuwa yuko tayari kumuwekea dhamana mchekeshaji huyo.

Msanii huyo ambaye ana marafiki zaidi ya milioni tano katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, picha aliyoweka ilipendwa na watu zaidi ya elfu sitini.

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam alidai kuwa msanii huyo hajui kazi yake na amevuka mipaka kwa kitendo alichofanya.

Hatua hiyo imepelekea watu kuhoji kama sheria inasemaje kuhusu ukamatwaji wa watuhumiwa na hata kosa lake ni lipi?

"Hivi sheria inasemaje kuhusu wito wa kwenda kituo cha polisi? Mitandao ya kijamii ina sifa ya kuwa njia mojawapo ya kumpatia mtu wito wa kufika kituo cha polisi?Je Idris anaweza kuwakilishwa kwenye wito huu na mwanasheria?" mtumiaji mmoja wa mtandao.

Inawezekana Sultan akahukumiwa kwa kosa la kosa la uharifu mtandaoni , sheria ambayo imekuwa ikipingwa na wanaharakati wengi nchini humo.

Hata hivyo hiki kinachotokea Tanzania sasa kwa msanii kushakiwa kwa kujeli kiongozi wa nchi au familia ya kiongozi.

Chanzo cha picha, TWITTER/VARIOUS

Tukio hili la kiongozi wa Afrika kufanyiwa masihala sio geni kwani mnamo June mwaka 2016, kundi kubwa la wanafunzi wa sekondari nchini Burundi walihukumiwa kwa kosa la kuharibu picha ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza.

Vijana hao walikabiliwa na adhabu kifungo cha miaka mpaka kumi jela.

Huku waangalizi wanasema maafisa wa serikali walianza kupambana na kile kinachoonekana kuongezeka kwa visa vya kuharibu picha ya rais katika vitabu vya wanafunzi shuleni.

Mamia ya wanafunzi, wengine wakiwa na umri mdogo wa miaka kumi na miwili walifanya maandamano kutokana na kamatakamata hiyo, lakini polisi hawakujali na kufyatulia risasi.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Bi Nyanzi alishtakiwa kwa kumtusi rais Yoweri Museveni, na mkewe Janet Museveni pamoja na marehemu mama yake Museveni, Bi Esteri Kokundeka kupitia Facebook

Huko nchini Uganda imempata mwanaharakati na mwalimu wa chuo kikuu cha Makerere nchini humo Dkt Stella Nyanzi ya unyanyasaji wa mtandaoni.

Dkt. Nyanzi ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa rais Museveni , alishtakiwa kwa makosa mawili, unyanyasaji wa kimtandao pamoja na mawasiliano ya udhalilishaji rais Yoweri Museveni, na mkewe Janet Museveni pamoja na marehemu mama yake Museveni, Bi Esteri Kokundeka, kupitia ujumbe alioutuma kwenye Facebook.

Lakini vilevile sio Afrika pekee inakutana na visa vya namna hiyo, huko Mareakani mchekeshaji aliyefanyia utani mwana wa Trump, Barron, asimamishwa kazi baada ya kuandika ujumbe uliomkejeli mtoto huyo kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Barron, 10, (kushoto) ndiye kitinda mimba wa Donald Trump

Mchekeshaji bi.Katie Rich aliandika ujumbe kwenye Twitter akisema: "Barron atakuwa mtu wa kwanza mshambuliaji hapa nchini aliyepokea elimu yake nyumbani."

Ujumbe huo wa mzaha unaonekana kutania suala la matumizi ya silaha Marekani, ambapo kumeripotiwa visa kadhaa vya raia wa Marekani kuwaua watu wengi kwa kuwapiga risasi.

Kinyume na ujumbe unavyoashiria, Barron hahudhurii masomo yake nyumbani bali husomea shule ya kawaida.

Bi. Rich alishutumiwa vikali mtandaoni kutokana na ujumbe huo na kuomba msamaha

Chanzo cha picha, Twitter