Mwanafunzi afariki baada ya kuchapwa viboko nchini Burundi

Adhabu ya viboko hairuhusiwi nchini Burundi lakini mwanafunzi kapigwa mpaka kufa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Adhabu ya viboko hairuhusiwi nchini Burundi lakini mwanafunzi kapigwa mpaka kufa.

Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14 huko nchini Burundi amefariki baada ya kupigwa na mwalimu wake, baba wa mtoto huyo ameiambia BBC.

Mtoto huyo, Chadia Nishimwe alipigwa viboko kwenye maeneo ya shingo na miguuni , kipigo ambacho kilimpelekea kutokwa damu puani na masikioni, alisema Jean-Marie Misago.

"Alikufa darasani mara baada ya kupigwa na mwalimu wake, na wakaenda kumtelekeza katika ofisi ya mwalimu mkuu," Bwana Misago alisema.

Mkuu wa shule alijaribu kumuwahisha hospitalini mtoto huyo wakati mtoto ameshakufa tayari, aliongeza baba huyo.

Unaweza pia kusoma:

BBC imejaribu kutafuta taarifa zaidi katika sekta ya elimu bila mafanikio.

Mtoto huyo aliuwawa siku ya jumanne na kuzikwa siku hiyo hiyo .

Nchini Burundi, adhabu ya kuchapwa kwa mwanafunzi ni kinyume na sheria ingawa bado wanafunzi wanachapwa.

Tukio kama hilo la mwalimu kumuua mwanafunzi lilitokea nchini Tanzania mwaka 2018 ambapo mwanafunzi mmoja wa darasa la tano katika shule ya Msingi Kibeta,manispaa ya Bukoba mkoani Kagera nchini Tanzania alidaiwa kupigwa na mwalimu wake mpaka kufariki kwa tuhuma ya kuiba mkoba wa mwalimu huyo.

Mara baada ya tukio hilo Waziri wa Elimu nchini Tanzania, Joyce Ndalichako amewataka watu wawe watulivu hadi upelelezi wa tukio hilo utakapomalizika.

"Shule ni sehemu salama sasa isitokee mtu aondoa hiyo dhana, hiyo ni bahati mbaya iliyotokea na isitafsiriwe kuwa shule sio mahali salama, Serikali itawashughulikia wale wote ambao wanahatarisha amani na usalama"Waziri Ndalichako aeleza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa na shirika la habari Tanzania,TBC wazazi kususia kuzika mwili wa marehemu kwa kudai kuwa ripoti iliyotolewa na daktari iliyosemwa kwamba mwanafunzi huyo alikuwa ana majeraha ya siku mbili kabla ya kupigwa na walimu huyo sio ya kweli.