Amnesty International yalaani uamuzi wa Tanzania kuzuia raia kuishtaki serikali Mahakama ya Afrika

Mahakama ya Afrika nchini Tanzania, ilisimamia kesi za kimbari za Rwanda Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mahakama ya Afrika nchini Tanzania, ilisimamia kesi za kimbari za Rwanda

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limesema uamuzi wa wa Tanzania kujitoa katika kifungu kinachowawezesha raia na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali kuishtaki serikali katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu inahatarisha ongezeko la ukandamizaji nchini humo.

Amnesty imesema kujitoa huko kunawanyima watu na mashirika mbali mbali uwezo wa kupata haki zao za kisheria.

Msemaji wa Amnesty barani Afrika , Japhet Biegon amesema ''kitendo hicho moja kwa moja kinageuka na kuwa kikwazo kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kutokwenda mahakamani kutafuta haki zao kwa makosa ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu, jambo ambalo ni dhahiri kuwa wanataka kukwepa wajibu wao.''

Mahakama hiyo makao makuu yake yapo mkoani Arusha, kaskazini mwa Tanzania. Na nchi hiyo sasa itakuwa ya pili baada ya Rwanda kujiondoa kwenye kipengele hicho cha mkataba ulioanzisha mahakama hiyo.

Huwezi kusikiliza tena
Amnesty International kulaani uamuzi wa Tanzania kuzuia wananchi na mashirika kuishtaki

Kwa muujibu wa shirika la Amnesty International, hatua hiyo inaweza kuzua wasiwasi kuhusiana na nchi hiyo ambayo rekodi za haki za kibandamu zimekuwa zikimulikwa ndani ya miaka michache iliyopita.

Katika barua kwa Umoja wa Afrika, ambao wanachama wake ndio waanzilishi wa mahakama hiyo, Tanzania ilielezea kuwa ilikuwa inajiondoa kwa kuwa mahakama hiyo imeshindwa kufanyia kazi maombi yake juu ya ruhusa ya watu na mashirika kushtaki serikali katika mahakama hiyo.

Takribani asilimia 40 ya kesi zilizofunguliwa katika mahakama hiyo ni dhidi ya Tanzania, licha ya kuwa nchi zaidi ya 50 za Afrika kuwa waanzilishi wa mahakama hiyo pia.

"Uamuzi umefanyika baada ya maamuzi kufikiwa kinyume na maombi yaliyowasilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," amesema Palamagamba Kabudi, waziri wa mambo ya nje wa Tanzania.

Tanzania iliiandikia mahakama ya Afrika mwaka 2010 ikitaka raia na mashirika kupeleka mashauri yao kwenye mahakama hiyo baada ya kupitia mfumo mahakama zote za ndani.

Amnesty inaamini kuwa, uamuzi huo wa Tanzania ni kielelezo kingine kuwa uhasama unaongezeka dhidi ya wanaharakati na watetezi wa hai za binadamu nchini humo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii