Mwanaume asiyekuwa na makazi afanya uhalifu ili afungwe

magereza

Chanzo cha picha, Getty Images

Hivi karibuni huko nchini Tanzania, kumekuwa na gumzo kuwa baadhi ya wafungwa walioachiwa kwa msamaha wa rais siku ya sherehe za uhuru kuripotiwa kufanya uhalifu ambao unaweza kuwarejesha gerezani.

Matukio hayo yametafsiriwa na baadhi kama namna ya watu hao kutaka kurejea gerezani. Kama ndiyo hivyo, basi mambo hayatofautiani sana hata kwenye mataifa yaliyoendelea pia.

Kijana mmoja nchini Ujerumani, ambaye hana kazi wala mahali pa kuishi aliamua kumgonga mtu aliyekuwa anaendesha baiskeli kwa maksudi ili tu aweze kufungwa gerezani na kupata mahali pa kuishi.

Mwendesha baiskeli ambaye alikuwa hajuani na mtu aliyemvamia ,alijeruhiwa vibaya .

Lakini mahakimu katika mji wa Oldenburg wanasema kuwa mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 62 alikuwa anatafuta makazi ya kuishi ndio maana aliamua kufanya tukio hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mahakama ilisikiliza namna ambavyo mwanaume huyo alivyopoteza ajira yake ya utaalamu wa sayansi ya komputa na hakuwa na namna nyingine ya kuishi kwa kuwa alikuwa amemaliza fedha zote za akiba katika mizunguko aliyofanya ulaya ya kutafuta ajira.

Wakati alipokamatwa , alikuwa hana nyumba bali alikuwa anaishi katika gari lake ambalo lilikuwa halina vibali vya kutembelea kwa muda mrefu.

Mwanaume huyo aliamua kuendesha gari na kumjeruhi mwanaume mwenye miaka 48 aliyekuwa anaendesha baiskeli.

Majaji wamemuhukumu kutokana na kitendo chake na kukubaliana na matakwa yake ya kutaka makazi ya kudumu jela, aidha wamedai kuwa bado anahaki ya kukaa gerezani kwa kuwa alifanya jaribio la kuua.

Mwendesha baiskeli bado anaugulia kutokana na athari alizopata kwa kuumia katika ajali hiyo.

Hicho kilichotokea Ujerumani , kinaweza kukaribiana na maamuzi ya baadhi ya wafungwa waliosamehewa na Rais John Magufuli katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa nchi hiyo, Desemba 9, 2019 .

Ambapo jumla ya wafungwa 5,533 ambao ni sawa na asilimia 15 ya wafungwa walisamehewa.

Lakini baadhi ya wafungwa wamejiingiza katika uhalifu mara tu walipotolewa huku mmoja wao akitaka kugoma kutoka gerezani.

Mfungwa huyo mmoja aliripotwa kugoma kutoka kwa madai kuwa hana mahali pa kwenda.

Mtazamo ambao ulionekana kwa wengi kuwa hawakuwa tayari kutoka na labda gerezani ni bora kwao kuliko hekaheka za uraiani.

Huku unyanyapaa kutoka jamii husika pia kuwa sababu ya baadhi ya wafungwa kuona bora kuendelea kuishi gerezani.