Wakati hali bado si shwari, kwa nini Tanzania yawarejesha wakimbizi Burundi?

Kwa miongo mingi tu Tanzania imekuwa msaada wa kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi na nchi jirani kama DRC na Rwanda.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Baadhi ya wakimbizi wa Burundi wakirejushwa kwao

Wahenga wanasema afadhali mkate mkavu kwa amani kuliko karamu katika nyumba ya ugomvi…

Baadhi ya raia wa Burundi waliamua kuacha karamu katika nyumba ya ugomvi kwa maana ya vurugu huko kwao na kukimbilia Tanzania kupata amani.

Walitamani kuishi katika makazi yao, wakitangamana na ndugu zao, wakifanya shughuli zao kwa namna yao lakini leo wanaishi kama wakimbizi kwa nchi isiyo yao Tanzania.

Kwa miongo mingi tu Tanzania imekuwa msaada wa kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi na nchi jirani kama DRC na Rwanda.

Ikiwa miongoni mwa nchi kinara Afrika kwa kuhifadhi wakimbizi.

Kambi 3 za wakimbizi zilizoko kaskazini mwa Tanzania, za Nduta, Mtendeli na Nyarugusu zina hifadhi wakimbizi zaidi ya laki tatu, wengi wao, ni kutoka nchi ya Burundi.

Waziri wa fedha na mipango wa Tanzania, Dr. Philip Mpango, alisema hivi karibuni kuwa jambo la muhimu ni amani, lakini hali hii iwe funzo kwa sababu kupitia vurugu na mapigano katika nchi jirani kama Burundi ndio kumesabisha idadi kubwa ya wakimbizi.

Pamoja na sababu zingine, vita vya wenyewe kwa wenyewe, ndiyo sababu kuu inayowakimbiza maelfu kwa maelfu ya wananchi wa nchi hiyo ya Burundi pamoja na nchi zingine kama DRC na Rwanda na kukimbilia Tanzania kutafuta amani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Baadhi ya wakimbizi wakaonyesha wasiwasi wa usalama wao pindi watakaporejeshwa huko Burundi.

Pamoja na yote, Tanzania imekuwa ikihaha kuwarejesha wakimbizi hasa wa Burundi makwao.

Makubaliano ya kuwarejesha wakimbizi wa Burundi yalifikiwa mwezi Machi mwaka 2018, kati ya pande pande tatu : serikali za Burundi, Tanzania na Shrika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR

Hatahivyo zoezi hilo lilipotangazwa rasmi, kuanza kutekelezwa Oktoba mosi mwaka 2019 , kwa kuanza kuwarudisha wakimbizi 2000 kila wiki kwa hiari, baadhi ya wakimbizi wakaonyesha wasiwasi wa usalama wao pindi watakaporejeshwa huko Burundi.

Upande wa serikali ya Burundi, haukuwa na shida ya kutekeleza makubaliano ya kurejesha wakimbizi wa nchi hiyo kutoka Tanzania, waziri wa mambo ya ndani wa Burundi, Pascal Barandagiye aliwahi kueleza hilo alipozungumza na wakimbizi wa Burundi kwenye moja ya kambi za Nduta na Mtendeli nchini Tanzania.

"Wale ambao wanataka kurejea Burundi, tunawatakia zoezi jema na wale ambao waliweza kunisikiliza yale niliyowaamabia, waweke nguvu na kujiandikisha waweze kurejea Burundi, tumewaandalia mazingira mazuri",Waziri wa Mambo ya ndani Burundi.

Hata hivyo, baadhi ya watu na mashirika mbalimbali yanayohudumia wakimbizi, yanaonesha kuwa na wasiwasi na zoezi hilo endelevu la kuwarejesha wakimbizi wa Burundi nchini mwao.

Mtazamo wa watu hao na mashirika ni kwamba mazingira hayajakaa sawa nchini Burundi kwa asilimia kubwa kuweza kufanikisha zoezi hilo kwa kiwango cha kuridhisha.

Hatua hiyo inamfanya waziri wa mambo ya ndani wa Tz, kutoa onyo.

Nguvu anayoisema , Waziri wa Mambo ya ndani, Kangi Lugola kuhusu Rais Magufuli hatanii, kwani mtazamo wa Rais huyo wa Tanzania ni kwamba, nchi hiyo haiwezi kusulubiwa kwa mzigo wa wakimbizi hasa wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

Kwa wananachi wa Watanzania, wenyewe zoezi la kuwarejesha wakimbizi wa Burundi makwao, wanalichukulia kwa hisia na mitazamo tofauti ambapo wapo wanaoona zoezi la kuwarejesha ni sawa, lakini wengine wana mtazamo tofauti.

Wadadisi wengi wanahoji, kama hali ya usalama haitatengemaa nchini Burundi, dhamira ya kurejesha wakimbizi wa nchi hiyo kutoka Tanzania, itakuwa na maana?

Waziri mkuu wa Tz, Kassim Majaliwa, anaeleza mkakati uliopo, wa kupunguza ama kumaliza wakimbizi, ni pamoja na kuimarisha usalama nchini Burundi…

Zoezi la kuwarejesha wakimbizi wa Burundi nchini mwao, kwa mujibu wa serikali ya Tz ni endelevu, limeanza, na litaendelea kwa kurejesha raia zaidi ya laki mbili wa Burundi.

Zoezi hili huenda likachukua mpaka miaka zaidi ya miwili, iwapo mpango wa kuwarejesha wakimbizi 2,000 kwa kila wiki hautabadilika.

Pamoja na kurejea makwao, hoja hapa, kwanini kuwepo kwa wakimbizi kila siku? Hakuna suluhu ya kudumu?