Tanzania yaongoza katika nyimbo kumi bora za Afrika Mashariki 2019

  • Roncliff Odit
  • BBC Swahili
msanii Harmonize

Chanzo cha picha, Instagram

Maelezo ya picha,

Msanii Harmonize

Sekta ya sanaa ya muziki imeshuhudia mabadiliko makubwa mwaka 2019.

Mojawapo ya taarifa kubwa mwaka huu ikiwa msanii Harmonize kujitosa nje ya kundi la Wasafi na mtindo mpya wa Gengetone kutetemesha sana nchini Kenya.

Licha ya yote hayo, wasanii tajika wa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati wamejitahidi kuwatumbuiza mashabiki kwa ngoma moto moto.

Lakini ni nyimbo zipi ambazo zilitetemesha sana chati za muziki mwaka huu?

Mwenzetu Roncliffe Odit anatathmini nyimbo 10, ambazo kwa mtizamo wake, ndio zilikuwa kubwa zaidi mwaka huu wa 2019…

Chanzo cha picha, Sailors

Maelezo ya picha,

Kikundi cha wanamuziki wa Sailors kilichoimba wimbo Wamlambez

Vilio vya uuuuwwwwwwi, vya kundi la Sailors kutoka Kenya vinafungua chati yangu katika nafasi ya kumi.

Vijana hawa kutoka mtaa wa mabanda wa Kayole jijini Nairobi wamebadili sera ya muziki wa kizazi kipya.

Wimbo wao 'Wamlambez' ni kama wimbo wa taifa, na kupelekea kuzaliwa kwa mdundo mpya wa Gengetone nchini Kenya, Wamlambez....

Katika nafasi ya tisa, naiweka Halleluyah ushirikiano wa Willy Paul na binti mrembo, malkia wa Bongo Flava, Nandy.

Utamu wa ajabu katika wimbo huu ambao hujui uuweke katika jedwali la nyimbo za injili ama za burudani tu.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Nandy, mwanamuziki wa Tanzania

Lakini ukweli ni kwamba weledi wa Willy Pozee katika kucheza na mistari hauna mfano wake.

Kisha ukiongeza umaridadi wa sauti ya Nandy, ah, acha nisiseme sana, Halleluyah...

Katika nafasi ya nane, Never Give Up yake Harmonize akizungumzia maisha yake ya shida ya zama za kale, kabla awe msanii tajika.

Huu ulikuwa wimbo wake wa mwisho ulionoga sana kabla ya kuihama lebo ya Wasafi na kuunda lebo yake mwenyewe ya Konde Gang. Ama kwa kweli, Never Give Up...

Turejee tena Kenya katika nafasi ya saba, Extravaganza ya Sauti Sol wakishikiana na Bensoul, Nviiri the Storyteller, Crystal Asige na kundi la Kaskazini, wote hao ni wasanii walio chini ya lebo yao ya mpya Sol Generation.

Mchanganyiko wa sauti tamu, na mpigo wa ajabu wa ala za muziki katika wimbo huu unakupatia utamu wa kipekee, yaani Extravaganza.

Chanzo cha picha, Ali Kiba/Instagram

Nafasi ya sita nitaipa Mshumaa yake Ali kiba.

Wimbo huu aliuachia mwezi mmoja tu uliopita. Ndio wimbo wake wa peke yake wa hivi karibuni zaidi, baada ya kufanya collabo kadhaa za kuwajulisha wasanii waliosajiliwa na lebo yake ya Kings Music Records.

Mshumaa ni wimbo ambao unaturudishia kumbu kumbu za King Kiba kama tunavyomfahamu.

Melody tamu na mistari yenye uzito, weee, washa Mshumaa...

Nafasi ya tano inasalia Tanzania, na wimbo Tamu wake Mbosso Khan, msanii wa kundi la Wasafi.

Sina mengi ya kusema kumhusu Mbosso, ila huyu kijana kabarikiwa mistari ilioiva, sauti tamu, na ushairi wa hali ya juu. Ama kwa kweli ni Tamu.

Katika nafasi ya nne nasalia ndani ya kundi la Wasafi na wimbo mpya wa Rayvanny I Love You.

Msanii huyu wa kundi la Wasafi amecheza na mistari, na kuachia melody safi sana iliyojaa mashairi ya kipekee. Mdundo wa pole pole unaenda kinyume sana na Rayvanny wa kitambo tuliyemjua kwa kufokafoka na midundo sawia na hip hop. Hata mimi nakwambia msomaji I Love You...

Sasa tugeukie nyimbo tatu ambazo ndizo kubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati.

Nafasi ya tatu inakwenda Uganda kwa wimbo Parte After Parte wake Big Tril.

Nilipouskiza mara ya kwanza, wimbo huu ulisikika kama mchezo tu. Lakini miezi minne tangu kuachiwa kwake, umekuwa wimbo mkubwa zaidi ya ulivyotarajika.

Mdundo wake wa club ukichanganya na hisia za sherehe zinazoambatana na wimbo huo zimefanyiza mchanganyiko ambao kila mtu anaucheza sasa. Parte After Parte...

Wimbo namba mbili Afrika Mashariki na Kati ni wake gwiji wa muziki wa Bongo Flava Diamond Platinumz, Inama, ambao amemshirikisha Fally Ipupa.

Wimbo huu uliachiwa Juni mwaka huu. Mdundo wake wa densi na video safi ya wacheza densi wa Wasafi wakiongozwa na Mose Iyobo unaifanya ngoma hii kupendeza na kuandaa burudani safi sana.

Yaani usiseme sana, wewe Inama...

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mwanamuziki wa Bongo Flava Diamond Platinumz

Na hatimaye wimbo namba moja, wimbo mkubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati...

Yope Remix ni wimbo wa msanii mkongomani Innocent Balume almaarufu Innoss B, ambaye ni muimbaji na dansa kutoka Goma, mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika remix ya wimbo wake Yope, Innoss B amemshirikisha Diamond na kuleta utamu wa mdundo wa DRC wa kusakata kiuno na melody tamu ya Bongo Flava.

Miezi mitatu tu tangu kuachiwa kwa wimbo huo, umetazamwa zaidi ya mara milioni 41 katika mtandao wa Youtube. Yope Remix ndio chaguo langu...