Tanzania yashiriki Afcon huku Kipchoge akivunja rekodi ya dunia

  • Yves Bucyana
  • BBC Africa, Kigali
Michael Olunga (kushoto) amekuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Michael Olunga (kushoto) amekuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Tanzania

Karibu sana katika makala maalumu ya matukio makubwa yaliyojiri katika ulimwengu wa michezo mwaka unaomalizika wa 2019 nikianza na kombe la Afrika la mataifa lililochezwa nchini Misri kwa mara ya kwanza fainali za kombe hilo zilishirikisha mataifa 24 .

Kwa mara ya kwanza Afrika mashariki ikawakilishwa na timu 4 ambazo ni Burundi iliyoshiriki kwa mara ya kwanza,Tanzania, Kenya na Uganda, lakini kubwa zaidi ilikuwa Tanzania kushiriki katika kundi moja na Kenya ambazo ni watani wa jadi hata kuanzia ngazi ya CECAFA.

Mbali na michuano mingine ya kombe la AFCON, Mchezo kati Kenya na Tanzania yao ulizungumzwa sana kama dabi ya Afrika mashariki.

Hatimaye, Kenya ikaibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 3-2 na kuwafurahisha mashabiki wa Kenya walioshuhudia pambano hilo:

Chanzo cha picha, CAF

Maelezo ya picha,

Samatta akiwa kwenye michuano ya AFCON 2019

Kwa upande wake nahodha wa Taifa Stars ya Tanzania Mbwana Samatta alihuzunishwa na jinsi walivyopoteza pambano hilo ilihali walikuwa mbele kwa bao 2.

Timu ya Tanzania imeshiriki michuano hiyo baada ya kipindi cha miaka 39 kupita bila ya taifa hilo kushiriki fainali za kombe la Afrika la mataifa:

Hatimaye timu nyingine zilizokuwa katika kundi hilo Senegal na Algeria zilikutana katika fainali na Algeria ikaibuka kidedea kwa kushinda bao 1 bila na kutawazwa mabingwa wa Afrika.

Maelezo ya picha,

Mwanariadha bora wa Kimataifa, Eliud Kipchoge

Mbali na soka, mwaka huu unaomalizika pia ulitawaliwa na riadha kubwa zaidi ni mwanariadha wa Kenya Eliud Kipchoge kuweka muda bora zaidi chini ya saa mbili katika mbio za Marathon katika Ineos .

Matukio mengine ya riadha, Urusi imefungiwa kwa miaka minne kushiriki michezo yoyote mikubwa ya kimataifa na wakala wa kupambana na dawa za kusisimua misuli (Wada).

Ina maanisha kuwa bendera ya Urusi haitapepea wala wimbo wao wa taifa wa nchi yao hautapigwa kwenye michuano kama ya Olimpiki ya mwaka 2020 na michuano ya kandanda ya kombe la dunia ya mwaka 2022 nchini Qatar.

Na mwisho kabisa, Kenya yamaliza ya pili baada ya Marekani katika mashindano ya riadha ya duniani.

Kama ilivyokuwa mwaka 2017 wakati wa mashindano kama haya, wakati yalipofanyika jijini London nchini Uingereza, Marekani imemaliza ya kwanza, huku Kenya ikiwa ya pili.

Marekani iliongoza kwa kupata medali 29, zikiwemo 14 za dhahabu, 11 za fedha na 4 za shaba.

Kenya ilimaliza mashindano hayo kwa kupata medali 11, zikiwemo tano za dhahabu mbili za fedha na nne za shaba.

Miongoni mwa wanariadha wa Kenya waliopata medali ya dhahabu ni pamoja na Hellen Obiri mbio za Mita 5,000 kwa upande wa wanawake na Conseslus Kipruto Mita 3,000 kuruka viunzi na maji.