Mzozo wa mpakani kati ya Uganda na Rwanda bado mwiba mchungu

  • Yves Bucyana
  • BBC Afrika, Kigali
Rais Paul Kagame na Yoweri Mseveni

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Yoweri Mseveni wa Uganda

Katika makala zetu maalumu za mwisho wa mwaka tunaangazia hali ya uhusiano mbaya kati ya Rwanda na Uganda, uhusiano ulioanza kuharibika mwanzoni mwa mwaka huu kufuatia Rwanda kufunga kituo cha mpaka cha Gatuna baina yake na Uganda.

Rwanda iliwakataza wananchi wake kuingia tena nchini Uganda .

Serikali ya Rwanda inaishutumu Uganda kuwanyanyasa raia wake wanaoishi ama kutembelea nchini Uganda na pia nchi hiyo kusaidia makundi ya waasi wanaotaka kuangusha utawala wa Rwanda.

Uganda inakanusha hayo na kwa upande wake kuishutumu Rwanda kutumia ardhi yake kwa ujasusi.

Maelezo ya picha,

Mpaka wa Uganda na Rwanda

Kumekuwepo na juhudi za mataifa ya Angola na Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo kupatanisha nchi hizo jirani lakini bado hazijazaa matunda.

Kuvunjika kwa uhusiano kati ya Rwanda na Uganda kulianza mwishoni mwa mwezi wa pili mwaka huu ambapo mamlaka ya mapato ya Rwanda ilifunga kituo cha mpaka wa Gatuna na kusimamisha maroli ya mizigo kutotumia tena mpaka huo kutokana na shughuli za ujenzi wa kituo hicho.

Hali hii ilisababisha biashara iliyokuwepo baina ya Rwanda na Uganda kukwama huku bei za bidhaa kutoka Uganda kupanda mara dufu katika masoko ya hapa Rwanda.

Wakati watu bado wakiwa wanajiuliza kilichokuwa kinaendelea, Rais Paul Kagame akaeleza kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na nchi ya Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita nchi ya Uganda ikitaka kuangusha utawala wake.

Akihutubia mkutano wa kitaifa Rais Kagame amesema mgogoro huo ulishika kasi mnamo miaka ya hivi karibuni kutokana na serikali ya Uganda kuunga mkono kundi la RNC linalopinga Rwanda na ambalo linatumiwa na Uganda kuwanyanyasa raia wa Rwanda wanaotembelea au wanaoishi nchini Uganda.

Nchi za ukanda wa maziwa makuu Angola na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo ziliingilia kati mgogoro huu na kujitolewa kupatanisha, Angola ikapokea mkutano wa Marais Kagame na Yoweri Museveni mjini Luanda mwezi Agosti.

Marais hao walisaini makubaliano ya kumaliza mgogoro huo na kuunda tume ya pamoja ya kutekeleza maazimio ya mkutano wao.

Maelezo ya picha,

Upande wa Rwanda mkakati wa kuwazuiya wananchi kwenda Uganda bado umeimarishwa

Mkutano wa kwanza wa tume ya pamoja iliyopendekezwa na kikao cha marais hao kutekeleza maazimio yao ulifanyika Kigali mwezi septemba.

Matokeo katika mkutano huo wa tume ya pamoja kilisomwa na mmoja wa wajumbe wa mkutano huo.

Mkutano wa pili ambao huenda ungeamua suala la kufunguliwa kwa mpaka wa Gatuna ulipangwa kufanyika mjini Kampala uliahirishwa hadi tarehe ambayo haijafahamika na hali ya uhusiano bado inaendelea kuwa mbaya.

Upande wa Rwanda mkakati wa kuwazuiya wananchi kwenda Uganda bado umeimarishwa hadi kuwapiga risasi wanaokiuka taratibu za mpakani.